Home Uncategorized WAZIRI MKUU ATEMBELEA NA KUKAGUA UJENZI HOSPITALI YA NAMTUMBO

WAZIRI MKUU ATEMBELEA NA KUKAGUA UJENZI HOSPITALI YA NAMTUMBO

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Januari 06, 2023 ametembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Namtumbo, Mkoani Ruvuma.

Akizungumza na wananchi wa eneo hilo Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya ili kusogeza huduma muhimu za kijamii karibu na wananchi.

Mheshimiwa Majaliwa amesema ziara katika hospitali hiyo ni kukagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Oktoba 18, 2022 alipotembelea hospitalini hapo na kuagiza kasoro zilizopo ikiwemo milango 10 iondolewe na kuwekwa mingine yenye viwango ifikapo Januari 4, 2023.

Kufuatia utekelezaji huo Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na utekelezaji wa maelekezo hayo ambapo hadi sasa jumla ya milango 67 kati ya 84 imeondolewa na kuwekwa yenye ubora na milango 15 kati ya 54 imewekwa katika majengo mapya ambayo yalikuwa hayajawekwa milango.

Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakuu wa Idara katika halmashauri zote nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa shughuli zote za kimaendeleo katika maeneo yao ili kuhakikisha fedha zinazoletwa na Rais Dkt. Samia kwa ajili ya ujenzi wa miradi zinatumika ipasavyo.

Mpaka sasa hospitali hiyo imepokea shilingi bilioni 4.2 kutoka Serikali kuu ambapo majengo 20 yameshajengwa, majengo 13 yamekamilika, majengo 5 yapo katika hatua za mwisho za ukamilishaji na 2 yapo kwenye hatua za upauaji na upigaji lipu.

Previous articleMAGAZETI YA LEO IJUMAA JANUARI 6 – 2023
Next articleBoT YABAINI KUONGEZEKA KWA UDANGANYIFU WA MIAMALA YA FEDHA MTANDANI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here