Home LOCAL WAJAWAZITO 309 NA WATOTO WACHANGA 1,200 WAMEPOTEZA MAISHA MWAKA 2022

WAJAWAZITO 309 NA WATOTO WACHANGA 1,200 WAMEPOTEZA MAISHA MWAKA 2022

Na. WAF – Pwani

Takwimu zinaonyesha kuwa kanda ya Mashariki Jumla ya akina mama wajawazito 309 na watoto wachanga 1,200 wamepoteza maisha katika kipindi cha mwaka 2022 Kanda ya Mashariki.

Hayo yamebainishwa leo na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Bi. Zuwena Jiri wakati akifungua kikao kazi cha tathimini ya mwaka na mapitio ya vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto chini ya miaka mitano kanda ya Mashariki kilichofanyika Mkoani Pwani.

“Takwimu hizi hazifurahishi hivyo kikao kazi hiki kitumike vizuri katika kufundishana, kubadilishana mawazo na kupanga mikakati ambayo itatusaidia katika kuhakikisha tunaboresha huduma za Afya ya uzazi na watoto wachanga katika kanda yetu ya Mashariki.” Amesema Bi. Jiri

Bi. Jiri Amesisitiza kuwa matatizo yanayochukua uhai wa wapendwa wetu yanaweza kuzuilika kwa asilimia 95 kama tukijipanga vyema toka kwa mama anapokuwa mjamzito.

“Tuipe elimu jamii yetu ili wajue umuhimu wa wajawazito kuwahi kliniki mapema ikiwa chini ya wiki 12 kwa lengo la kujikinga yeye pamoja na mtoto na kama kuna hatari inayotaka kujitokeza basi iwahiwe mapema.” Amesema Bi. Jiri

Pia, amewasisitiza watoa huduma wahakikishe wanatoa huduma zote zinazotakiwa kwa ubora ili waweze Kubaini wajawazito wenye matatizo na kuyashughulikia mapema.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akinamama Dkt. Ulimbakisye MacDonald kutoka Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto wakati akitoa salamu za Wizara ya Afya amesema katika huduma za afya ya uzazi kumekuwa na ongezeko kubwa la akinamama wanaohudhuria kliniki mara nne na zaidi kwenye kliniki ya wajawazito toka 51% (TDHS 2015/16) mpaka 86% kwa takwimu za mwaka 2022.

“Vilevile, kiwango cha wajawazito wanaojifungua kwenye vituo vya kutolea huduma kimeongezeka toka 63% (TDHS 2015/16) mpaka 80% (DHIS2-2020).” Amesema Dkt. MacDonald

Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitekeleza makubaliano ya kimataifa ikiwemo azimio la Malengo Endelevu ya Milenia na Mkakati wa Dunia Kuhusu Afya ya Akinamama na Watoto wachanga (2016-2030).

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here