Home LOCAL TEF: MWAKA 2023 NI WA MAGEUZI MAKUBWA KATIKA SEKTA YA HABARI NCHINI

TEF: MWAKA 2023 NI WA MAGEUZI MAKUBWA KATIKA SEKTA YA HABARI NCHINI

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile amesema kuwa mwaka 2023 utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya habari ikiwamo kukamilika kwa mchakato wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini ya mwaka 2016.

Balile ameyasema hayo kwenye mahojiano maalum na mwandishi wa Mtanzania Digital, na kusema kuwa TEF kwa kushirikiana na wadau wa habari tayari wamekamilisha kile walichopaswa kufanya.

“Ni matarajio yetu kwamba mwaka huu wa 2023 utaleta mageuzi katika tasnia ya habari.

“Sisi huku kwenye mikutano ya wadau tumeshamaliza ambapo kikao cha mwisho tulifanya Novemba 21, 2022, baadae tukaongeza na Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 lililofanyika Desemba 18, 2022.

“Hivyo kilichobaki ni Mswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kuwasilishwa bungeni baadae mwezi huu

“Hivyo, tunaamini kuwa mawazo ya wadau ambayo tulikubaliana katika maeneo yote haya ndiyo yatakayokuwemo katika mswaada huu unaokwenda kuwasilishwa bungeni Januari hii,” amesema Balile.

Balile amesema kuwa matarajio ya wadau wa habari ni kuona mswada huo wa mabadiliko ya sheria ukisomwa bungeni Januari 31, mwaka huu.

“Kwanza kabisa utapitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kisha utajadiliwa na Kamati ya Makatibu Wakuu na baada ya hapo utajadiliwa na Kamati ya Baraza la Mawaziri.

“Ukitoka hapo utajadiliwa na Baraza la Mawaziri, tunarajia itakuwa kati ya Januari 13 na 14, matazamio yetu ni kwamba utasomwa bungeni kwa mara ya kwanza Januari 31, mwaka huu kisha tutakutana na wadau kuzungumza na wabunge baadae utasomwa kwa mara ya pili na utajadiliwa,” amesema Balile.

Balile amesema kwamba kupitia kauli ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, aliyotoa siku ya Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 mswada huo utawasilishwa bungeni katika bunge linalokuja.

“Kwa kauli ile ya Mheshimiwa Waziri tunaimani kuwa mswaada huo utaingia katika bunge hili la Januari na maisha mengine yaendelee,”amesema Balile.

Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya Sera na Sheria nyingine katika sekta ya habari amesema kuwa hizo wataziona mbele ya safari.

Alichosema Waziri Nape Desemba 18, 2022 akizunumza katika Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022, Waziri Nape alisema kuwa Serikali inampango wakurekebisha sekta ya habari kupitia mfumo wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kuunganisha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010.

Waziri Nape alisema hatua hiyo inatarajiwa kuleta uratibu madhubuti wa sekta hiyo na umoja kati ya wahusika katika magazeti, mitandao ya elektroniki na kijamii kwa kuwa zote ziko chini yake.

“Pamoja na kupitia upya sera ya nchi ya vyombo vya habari, serikali inapanga kuunganisha sheria zinazohusu masuala ya vyombo vya habari na utangazaji, kwa kuwa zote mbili sasa ziko chini ya wizara moja.

“Ninathibitisha kuwa serikali itatuma bungeni kwa ajili ya kupitia marekebisho ya vifungu vya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 Januari mwakani(mwaka huu),” alisema Waziri Nape.

Upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Samson Kamalamo akizungumza hivi karibuni alisema mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari itakuwa mwanzo wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyopo katika sekta ya habari.

“Hii haitakuwa mwarobaini, isipokuwa itakuwa mwanzo wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyopo katika sekta ya habari na kuiboresha. Lakini pia, tujifunze kwa wenzetu wamefanikiwa vipi, tusijifungie ndani,” alisema Kamalamo.

Kwa mujibu wa ratiba vukao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vinatarajia kuendelea Januari 31, mwaka huu jijini Dodoma.

Previous articleMINADA MADINI YA VITO MBIONI KUANZA
Next articleRAIS DKT. SAMIA AFANYA UTEUZI WA VIONGOZI MBALIMBALI LEO JANUARI 05 –  2023
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here