Na Dotto Mwaibale,Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amemwagiza aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda kuwatafuta, kuwakamata na kuwaweka ndani waliokuwa viongozi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Walimu Iramba (CHAMWAI) kutokana na kushindwa kuwalipa walimu fedha zao zaidi ya Sh. Milioni 300.
Alisema viongozi hao wakikamatwa wafikishwe kwenye kikao kitakachofanyika siku ya Jumanne wiki ijayo kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kujibu tuhuma zinazowakabili.
Serukamba alitoa agizo jana wakati akizungumza na walimu zaidi 100 ambao walifika ofisini kwake kulalamika kutolipwa fedha hizo tangu mwaka 2012.
“DC nataka unitafutie wale viongozi wa zamani wa CHAMWAI kwa kuwakamata uwatie ndani mpaka tutakapokutana ili tuje tukutane nao Jumanne,” alisema.
Alisema katika kikao hicho pia wawepo pia maafisa ushirika walioshiriki jambo hilo tangu mwanzo, wakurugenzi wa halmashauri za Iramba na Mkalama, waweka hazina na viongozi wa sasa wa CHAMWAI.
“Nataka tupate mwelekeo mzuri tangu chama kilipoanzishwa fedha zilizokuwa zinachangwa zilikuwa zinapelekwa wapi na zilivyoanza kutoka zilikuwa zinakwenda wapi,” alisema.
Serukamba alisema katika chama hicho kuna matatizo mfano katika moja ya nyaraka za kuomba mkopo alisaini Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida wakati chama hicho kipo Wilaya ya Iramba.
Naye Mwalimu Nalogwa Temaec akizungumza kwa niaba ya walimu wenzake alimweleza Mkuu wa Mkoa alisema walianza kuchangia Sh.10,000 kila mwezi ambazo zilikuwa zikikatwa moja kwa moja kwenye mishahara yao na kuingizwa kwenye akaunti za chama.
“Tulikuwa tunaweka fedha zetu na kukopa,wakati tunakopa tulikuwa tunarudisha kwa ‘interest’ tukiwa na maana baada ya kustaafu kazi tutalipwa fedha zetu na chama wakati tukisubiri mafao ya serikali,” alisema.
Alisema tatizo lilianza kujitokeza baada ya wakurugenzi wa halmashauri kuingia tamaa na kuanza kuchukua makatibu ya fedha za chama zilizokuwa zinachangwa na wanachama na kuanza kuzitumia kwa kazi nyingine.
Kwamujibu wa ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) imeleza kuwa Kamati ya Mikopo ya chama hicho haikutekeleza majukumu yake ipasavyo kwani ikitoa mikopo bila kufuata utaratibu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akielekezwa jambo na walimu hao kabla ya kuanza kufanya kikao nao.