Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amelaani vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyofanywa na wananchi katika Shamba la Miti Buhindi lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Mkoani Mwanza.
Ametoa kauli hiyo wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Wilaya ya Sengerema ikiwa ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Miaka 46 ya Chama cha Mapinduzi.
“Wananchi wa Sengerema na Buchosa nimesikitishwa sana na kitendo mlichokifanya kwenye Shamba la Miti Buhindi kwa kuwa mmechoma kambi ya askari na kuunguza baadhi ya maeneo ambayo tunapanda miti na kuhifadhi misitu ya mazingira asili” amesisitiza Mhe. Masanja.
Amewaelekeza wananchi hao kutunza mazingira ya shamba hilo kwa kuwa ndilo linalofanya kuwepo na hali ya hewa nzuri ikiwemo upatikanaji wa mvua na linatunza vyanzo vya maji.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi kinara katika kukamilisha miradi ya maendeleo ambayo mwanzilishi wake aliiacha katika Mkoa wa Mwanza.
“Takriban bilioni 700 zimeletwa kwenye Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kukamilisha miradi ya kimkakati kama ujenzi wa stendi ya Nyamhongolo, Stendi ya Nyegezi, Daraja la Kigongo-Busisi, ujenzi wa meli na ukamilishaji wa miundombinu ya barabara.
Amesema sambamba na hilo Mheshimiwa Rais ametoa fedha za utekelezaji wa miradi katika Sekta mbalimbali kama elimu ambapo madarasa mengi yamejengwa pamoja na vituo vya afya.
“Tumpe nini Rais wetu zaidi ya upendo ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.” Mhe. Masanja amesema.