Home LOCAL “HAKIKINI NAMBA KUEPUSHA UHALIFU” – NAIBU WAZIRI KUNDO 

“HAKIKINI NAMBA KUEPUSHA UHALIFU” – NAIBU WAZIRI KUNDO 

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Kundo Andrea Mathew (MB) akizungumza katika mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kijiji cha Katurukila kilichopo Kata ya Mkula katika Jimbo la Kilombero Mkoa wa Morogoro katika ziara yake ya kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa TBC na uhakiki wa Anwani za Makazi Januari 7, 2023

Mhandisi wa Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Mashariki, Fredy Bushesha akijibu maswali ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Katurukila kilichopo Kata ya Mkula, Jimbo la Kilombero mkoani Morogoro wakati wa ziara Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Kundo Andrea Mathew (MB) ya kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa TBC na uhakiki wa Anwani za Makazi, Januari 7, 2023.

(Picha na John Manollo)

Na: Immaculate Makilika – WHMTH

Watanzania wameaswa kuhakiki namba zao za simu walizozisajili ili kuepusha uhalifu unaoweza kufanywa kupitia namba hizo.

Akizungumza hivi karibuni katika mkutano na wananchi wa Kijiji cha Katurukila kilichopo Kata ya Mkula, Jimbo la Kilombero mkoani Morogoro, wakati alipokuwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa redio TBC na uhakiki wa Anwani za Makazi.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa, Mhandisi Kundo Mathew amesema “Wananchi pigeni *106# na kufuata maelekezo ili muweze kuhakiki namba zenu za simu mlizozisajili kupitia Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na endapo mkigundua kuna namba hamzitambui na zimesajiliwa na vitambulisho vyenu, nendeni kwenye vituo vya watoa huduma ili muweze kuzifuta kwa kuwa wahalifu hutumia namba hizo zenye usajili wa watu wengine kufanyia uhalifu” .

Pia, Naibu Waziri Kundo, amewataka Watanzania kuwa makini wakati wa kufanya miamala mbalimbali kupitia simu zao za mkonono kwa kutotuma fedha kwa mtu bila kujiridhisha kwa vile kumekuwepo na wahalifu wanaoiba fedha kupitia mitandao ya simu.

Kuhusu kupokea jumbe zenye matusi au utapeli kupitia simu za mkononi, Mhandisi wa Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Mashariki, Fredy Bushesha amesema kuwa kutuma ujumbe wa matusi au utapeli kwa mtu ni kosa kisheria na hivyo mwananchi anapopata changamoto hiyo anatakiwa kuripoti neno utapeli kwenda namba 15040 au matusi kwenda namba 15040 ili mhusika aweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Amefafanua “Ikiwa mtu amepokea ujumbe wa matusi basi anatakiwa kuandika neno matusi na kutuma namba 15040, kisha itarudisha mrejesho na baada ya hapo unatakiwa kwenda kuripoti Kituo cha Polisi katika Kitengo cha Usalama wa Kimtandao ili namba iliyotumika kutuma ujumbe wa matusi isitishwe”. Amesema Mhandisi Bushesha.

Ameongeza kuwa baada ya uchunguzi kufanyanyika namba iliyotumika itafungwa sambamba na Kitambulisho cha Taifa kilichotumika kusajili namba hiyo hivyo mhusika hataweza kupatiwa huduma mbalimbali kwa kutumia Kitambulisho hicho cha Taifa.
Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here