Home LOCAL DC ATOA SIKU 10 KWA WALIOVAMIA BONDE LA MTO KILOMBERO

DC ATOA SIKU 10 KWA WALIOVAMIA BONDE LA MTO KILOMBERO

Mkuu wa wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro Bi. Hanji Godigodi ametoa siku 10 kuanzia Desembe 31,2022 kwa wafugaji, wakulima na wavuvi waliovamia eneo la kitalu cha uwindaji cha Mlimba Northern kilichopo ndani ya Bonde la Mto Kilombero kuondoka.

Maji ya mto Kilombero yanategemewa kwa kiasi kikubwa katika mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere,ambapo kukamilika kwake linatarajiwa kuzalisha megawati 2115 ambazo zitamaliza adha ya nishati ya umeme nchini.

Bi. Godigodi ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika kitalu cha uwindaji cha mwekezaji cha Kilombero Northern Safari ambacho kipo ndani ya kitalu cha Mlimba Northern ambapo alijionea uharibifu mkubwa uliofanywa na wakulima, wafugaji pamoja na wavuvi kwenye kitalu hicho kwa kukata miti na kuanzisha mashamba makubwa ya mahindi na ufuta huku wengine wakiweka makazi ya kudumu bila ya kuhofia wanyama wakali waliopo kwenye kitalu hicho.

Alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi wachache wanahujumu uchumi wa nchi, kwani uharibifu unaofanywa kwenye vyanzo vya maji unaathili moja kwa moja uwekezaji mkubwa wa mabilioni ya fedha uliofanywa na Serikali katika Mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere lililopo Rufiji mkoani Pwani.

“Zaidi ya Tilioni 6.5 zimewekezwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, sisi kama wanakilombero tupo tayari kwa namna yeyote kupambana na kikundi cha watu wachache wanaotaka kutuharibia taswira yetu na tuonekane ni waharibifu wa vyanzo vya maji” . alisema DC Godigodi.

“Tupo tayari kusafisha wafugaji wote pamoja na hao wakulima waliovamia eneo hili lengo ni  kuhakikisha mito yote iliyopo kwenye Bonde la mto Kilombero inarudi kwenye hali yake ya kawaida na maji ya kutosha yanaenda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere” . Aliongeza DC Godigodi. 

Alisema baada ya muda uliotolea kutoka kwa hiyari kwenye maeneo hayo Serikali wilayani humo haitomuonea huruma mwananchi yeyote kwani Mhe.Rais alishatoa tamko la kulinda vyanzo maji.

Kiongozi wa doria  Kitalu cha uwindaji cha Kilombero Northern Safari Bw. James Bebe alisema kutokana na uharibifu mkubwa wa ukataji wa miti na uanzishwaji wa mashamba makubwa kwenye kitalu hicho umepelekea wanyama kukosa maeneo ya kuishi na kutoa mwanya kwa majangili kuweza kutekeleza uharifu kwa njia rahisi zaidi.

“Uvamizi wa wakulima na wafugaji ndani ya kitalu cha Mlimba Northern ni mkubwa sana hali inayosababisha vyanzo vya maji kukauka pamoja na wanyama kutoweka kwani mifugo imekuwa mingi sana ndani ya kitalu” alisema Bw. Bebe. 

Pia alilishukuru jeshi la polisi kupitia kituo cha polisi Mlimba, TAWA, TANAPA pamoja Halmashauri ya Mlimba kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa katika kuhakikisha wavamizi na majangili wanakwisha kabisa katika kitalu hicho.

Awali akitoa elimu kwa wananchi wa kijiji cha Idundembo juu ya makosa mbalimbali na hatua zitakazochukuliwa na waharifu mkuu wa kituo cha Polisi Mlimba Donati Mhina aliwata wakazi wa vijiji vinavyozunguuka kitalu cha Mlimba Northern kuacha tabia ya kulima na kupeeleka mifugo yao ndani ya kitalu hicho kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

“Kukata miti bila ya kibali cha mamlaka husika, kufanya shughuli za kibinaadamu mita 60 ndani ya vyanzo vya maji ni kosa na limeanishwa kwenye sheria ya mazingira, hivyo kutokujua sheria hakukuruhusu wewe kutenda kosa”. Alisema Mkuu wa kituo cha Polisi Mlimba.

 Kwa upande wao wananchi waishio pembezoni mwa kitalu hicho walisema chanzo cha uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji unaofanywa wakulima na wafugaji kwenye Bonde hilo ni viongozi wa vijiji na kata  kwani wamekuwa wakiwakalibisha wageni na kuwaonyesha maeneo ambayo yamehifadhiwa na kuwalipisha fedha kuanzia 1,000, 000.

Bi. Shukrani Dononda ni mkazi wa kijiji cha Idundembo alisema viongozi wa vitongoji wamekuwa wakichukua fedha za wakulima na wafugaji jamii ya Kisukuma na kuwapelekeka kuwaonyesha maeneo kwenye kitalu cha uwindaji cha Mlimba Northern.

“Changamoto ipo kwa viongozi wetu japokuwa wananchi tumekuwa waoga kuweka wazi swala hili, hawa viongozi wa chini kama wangekuwa wanachukua hatua kwa watu ambao wanavamia maeneo yaliohifadhiwa basi wengine wasingiweza kuendelea kuvamia lakini hao vingozi wetu hawachukui hatua na wengine wana hadi mashamba yao huko kwenyekitalu”. Alisema Bi. Shukran mkazi wa Idundembo.

“Hawa viongozi ndio wanafanya watu waingie kule kuanzia viongozi wa vitongoji, vijiji, kata, watendaji pamoja na wale wa chama wanaogombea nafasi za kuchaguliwa  wakiwemo Madiwani na viti maalum wamekuwa wakipiga kampeni kupitia kugawa mashamba huko kwenye vyanzo vya maji”. Aliongeza.

Previous articleADC WAMPONGEZA RAIS SAMIA KUKUTANA NA VYAMA VYA SIASA NCHINI
Next articleMAGAZETI YA LEO JUMANNE JANUARI 3-2023
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here