Home LOCAL ADC WAMPONGEZA RAIS SAMIA KUKUTANA NA VYAMA VYA SIASA NCHINI

ADC WAMPONGEZA RAIS SAMIA KUKUTANA NA VYAMA VYA SIASA NCHINI

KATIBU Mkuu wa Chama cha ‘Alliance For the Democratic Change’ Doyo Hassan Doyo amesema kitendo cha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuitisha mkutano na vyama vya siasa kinapaswa kupongezwa kwa kuwa kinahimarisha afya katika siasa za hapa nchini.

Akizungumza Dar es Salaam leo Doyo amesema hatua hiyo ya Rais Samia, ni wazi imeonyesha dhamira yake ya kweli kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika siasa hususani kwa vyama vya upinzani na kwamba kwa kuliona hivyo ameona ni vyema kukaa nao pamoja na kuzungumza.

Rais Dkt Samia Suluhu Hassan hapo kesho anatarajia kukutana na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa katika mkutano unaotarajiwa kufanyika katika Ikulu ya Magogoni, mkutano ambao baadhi ya wadau wa masuala ya siasa nchini akiwemo Katibu huyo wa ADC wamesema unaashiria jambo jema ikizingatiwa ni mwanzo tu wa mwaka.

“Ukweli binafsi nimefarijika na hatua ya Rais Samia kuitisha mkutano huu mapema kabisa kwa mwaka, hizi ni dalili tosha kuwa lengo ni kuona tunakuwa na mipango ya uhakika kwa kila mmoja wetu katika siasa, sisi kama chama cha siasa ambao pia tutashiriki mkutano huo tunaipongeza hatua hii” alisema Doyo

Amesema wao kama ADC watahakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuitikia wito huo na kwenda kutoa mchango wa mawazo yao pale watakapopewa nafasi,  lengo ni kuona hali ya kisiasa nchini inahimarika kama ambavyo imeanza kujionesha hivi karibuni tangu Rais Samia Suluhu Hassan ashike madaraka ya kuongoza nchi.

Aidha amewataka viongozi na wanachama wa vyama vingine vya siasa kuhakikisha kwa nafasi zao pia wanajitokeza na kwenda kushiriki mkutano huo ulioitishwa na kiongozi huyo na mkuu wa nchi na kwenda kuwasilisha wale yote waliyonayo hatua itakayosaidia wapate majibu juu ya yale wanayaona hayastahili au yaboreshwe ndani ya siasa.

Amesema kitendo cha kutojitokeza katika mkutano huo kitawafanya kujinyima haki wao wenyewe, suala ambalo halitosaidia kuondoa malalamiko waliyonayo sambamba na kuwanyima haki wanachama wao.

Previous articleMAGAZETI YA LEO JUMATATU JANUARI 2-2023
Next articleDC ATOA SIKU 10 KWA WALIOVAMIA BONDE LA MTO KILOMBERO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here