Home LOCAL WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO KWA WATUMISHI WA HALMASHAURI NCHINI

WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO KWA WATUMISHI WA HALMASHAURI NCHINI

*_Awataka kwenda vijijini kuwasikiliza wananchi_*

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi kwenye Halmashauri zote nchini kutenga muda wa siku tatu kati ya siku za kazi kwenda vijijini ili kutatua changamoto za wananchi.

Amesema kuwa ni lazima watumishi wa umma wajue wajibu mkubwa ni kuwatumikia wananchi na kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye maeneo yao.

Amesema hayo leo Disemba 16, 2022 wakati wa kikao cha pamoja na watumishi wa umma wa Halmashauri za mkoa Rukwa ambako alikuwa kwenye ziara ya kikazi.

Amesisitiza kuwa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona kila mtumishi wa umma anawajibika katika kuwatumikia watanzania “Hawa wananchi wamesambaa katika Wilaya na halmashauri, tumejenga majengo ya ofisi sio lazima wananchi waje humo kupata huduma, wapo wengine hawawezi kuja hapa lakini wanahitaji Serikali yao inahudumie”

Aidha, Mheshimiwa amewataka viongozi katika halmashauri kuhakikisha wanasimamia watumishi kutokaa ofisini wiki nzima badala yake waende vijijini kwani huko ndiko wananchi walipo ili wawasikilize na kuwatumikia.

Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato, Waziri Mkuu amewataka watumishi wanaosimamia eneo hilo kufanya makadirio yenye uhalisia na kutambua vyanzo vyote ambavyo vinaweza kuingiza mapato “lazima mfanye tathmini eneo fulani linaweza kuwaingizia kiasi gani, kwa siku, kwa mwezi au kwa mwaka”

“Tunapotaka kukusanya mapato ya ndani anzeni kwa kubaini vyanzo na msiwaachie wakuu wa idara pekee “ Meya na wenyeviti wa halmahauri tushiriki kikamilifu, watendaji wa vijiji na kata hata watumishi wengine, tukishabaini turudi kusimamia sote”

Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia amewekea nguvu katika eneo la makusanyo “hakuna haja ya kutumia nguvu kubwa katika hili muhimu ni kusimamia, Serikali imeagiza kukusanya kielektroniki, tufanye hivyo, tumieni mashine zetu za POS”

Awali akikagua kituo kikuu cha mabasi Sumbawanga kilichopo eneo la Katumba Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Jacob Mtalitinyi kukutana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ili kuweka utaratibu wa kituo hicho kilichogharimu shilingi bilioni 7.9 kianze kutumika.

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia ameridhia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga “ Viwanja vitatu vya Mara (Musoma mjini), Shinyanga na hapa Sumbawanga vipo kwenye mpango wa kujengwa, kile cha Lindi kitajengwa na mradi wa gesi, Rais wetu anajua matakwa ya watanzania”

Katika hatua nyingine Jana (Disemba 15, 2022) wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa chuo cha Ualimu Sumbawanga kilichopo katika kijiji cha Pito, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameagiza kuwa ujenzi wa vyuo vya VETA nchini usimamiwe na makatibu tawala wa mikoa badala ya kusimamiwa na VETA mkao makuu.

amesema kuwa kufanya hivyo kutawezesha vyuo hivyo kuwa na usimamizi wa karibu hivyo kukamilika kwa wakati na viwango stahili. “Narudia tena, VETA wabadilishe mifumo yao ya ujenzi vyuo na visimamiwe na Makatibu Tawala wa mikoa kama kuna mtumishi wa VETA ataletwa atakuwa chini ya usimamizi wa Katibu Tawala wa mkoa ili uratibu uwe jirani zaidi”

Previous articleMAJALIWA AKAGUA KITUO KIKUU CHA MABASI SUMBAWANGA
Next articleWANASHERIA, WAENDESHA MASHTAKA NA WAPELELEZI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII WAPATIWA MAFUNZO JIJINI MWANZA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here