Home BUSINESS CHUO CHA TAIFA CHA UTALII (NCT) KUFANYA MAHAFALI YA 20 JIJINI DAR

CHUO CHA TAIFA CHA UTALII (NCT) KUFANYA MAHAFALI YA 20 JIJINI DAR

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dk.Frolian Mtey (wa pili kushoto) akijadiliana jambo na  Mkurugenzi wa Mafunzo na shughuli za Kitaaluma wa Chuo hicho  wa  Jesca William (wa kwanza kushoto) katika Kongamano la 2 la kitaaluma (convocation) lililofanyika katika chuo hicho Disemba 1,2022 Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mafunzo na shughuli za Kitaaluma wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Jesca William akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake katika hafla hiyo.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dk.Frolian Mtey akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake ya utangulizi kumkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Katibu Mtendaji wa TOURISM CONFEDERATION OF TOURISM (TCT) Bw. Richard Rugimbana akizungumza katika Kongamano la 2 la kitaaluma (convocation) la Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Jijini Dar es Salaam.

PICHA ZA WASHIRIKI WA HAFLA HIYO.

(PICHA ZOTE NA: HUGHES DUGILO)

Na: Hughes Dugilo, DAR

Imeelezwa kuwa mchango wa Serikali katika kuhakikisha utalii unakua nchini, imeongezeka hadi kufikia watalii 922,692 kwa mwaka 2021 ambao ni sawa na ongezeko la asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka 2020.

Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa TOURISM CONFEDERATION OF TOURISM (TCT) Bw. Richard Rugimbana alipokuwa akizungumza katika Kongamano la 2 la kitaaluma (convocation)  liliofanyika Disemba 1,2022 Jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya shamra-shamra kuelekea katika Mahafali ya 20 ya Chuo cha Taifa cha utalii (NCT) yatakayofanyika Disemba 02,2022 Jijini humo.

Amesema kuwa hivi sasa mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kwa asilimia 83 hadi kufikia Dola za Marekani 1,310.34 milioni kutoka Dola za Marekani 714.59 milioni zilizopatikana mwaka 2020. Wakati wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliongezeka hadi Dola za Marekani 199 mwaka 2021 kutoka Dola za Marekani 152 mwaka 2020.

“Kipekee kabisa nimshukuru Rais wetuMhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha utalii unaimarika ikiwemo uzinduzi wa filamu ya Tanzania: ‘The Royal Tour’ ambayo imesaidia kuitangaza Tanzania na vivutio vilivyopo lakini pia kuleta hamasa kwa watalii kutembelea nchi yetu, ambapo tumeshuhudia watalii wakija kwa wingi nchini” amesema Rugimbana.

Amesema Sekta ya utalii imeendelea kuchangia katika Pato la Taifa (GDP) kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni ambapo kwa kupitia utalii, ajira, nishati, elimu, utafiti, utamaduni, burudani na tiba sekta hiyo imeendelea kuchangia takriban asilimia 25 ya fedha za kigeni na zaidi ya asilimia 17 katika Pato la Taifa.

“Nitumie nafasi hii tena kuipongeza Serikali kupitia Wizara yake ya Maliasili na Utalii kuweza kuandaa Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani-Kamisheni ya Afrika (UNWTO) uliofanyika Oktoba 5-7, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Gran Melia jijini Arusha ukiwa na kauli mbiu “Kuujenga Upya Utalii Stahimilivu wa Afrika kwa Maendeleo Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii”.

“Mkutano huu ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO), Zurab Pololikashvili,  Mawaziri na viongozi wenye dhamana ya kusimamia masuala ya utalii kutoka Nchi Wanachama wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika. Pamoja na masuala mengine Mkutano huu ulilenga kuitangaza Tanzania na hivyo kusaidia kuchangia ongezeko la idadi ya watalii na wawekezaji nchini”

“Hii ni fursa kwetu kuendelea kuimarisha na kuboresha biashara za utalii hususan uboreshaji utoaji huduma kwa kuongeza idadi ya watoa huduma wenye weledi na sifa stahiki kama ambavyo tunashuhudia idadi kubwa ya wahitimu kutoka Chuoni kwetu” amesema.

Awali akizungumza alipokuwa akitoa salamu za utangulizi  Mkurugenzi wa Mafunzo na shughuli za Kitaaluma wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Jesca William amesema kuwa lengo la Chuo hicho kufanya kongamano hilo ni kutoa fursa kwa wadau kukutana na wanafunzi, kutambua na kutunuku zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika taaluma pamoja na wanafunzi kupata fursa ya kusikia toka kwa wataalamu wabobezi wa sekta nzima ya utalii hususani wale waliomaliza katika chou hicho.

“Tunategemea kuwa na mahafali ya 20 yatakayofanyika Disemba 1, 2022 katika ukumbi wa mwl Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. aidha chou kimetambua umuhimu wa kufanya Kusanyiko la kitaaluma “Convocation” kabla ya mahali hayo ili kutoa fursa kwa wadau kukutana na wanafunzi, kutambua na kutunuku zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika taaluma pamoja na wanafunzi kupata fursa ya kusikia toka kwa wataalamu wabobezi wa sekta nzima ya utalii” amesema Jesca.

Pia katika hafla hiyo baadhi ya wanafunzi waliomaliza katika chuo hicho walitoa shuhuda zao kuelezea namna walivyofanikiwa  kutokana na ujuzi walioupata katika chou hicho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here