Afisa Ukaguzi wa TASAC Gabriel Manase (kulia) akizungumza na wananchi mbalimbali katika zoezi maalum la utoaji wa elimu ya ulinzi, usalama na utunzaji wa mazingira lililofanyika katika wilaya ya Ifakara Mkoani Morogoro. (katikati), ni Maulid Nsalamba, na (wa pili kutoka kushoto), ni Afisa uhusiano mwandamizi wa TASAC Amina Miruko.
Maafisa ukaguzi na udhibiti wa vyombo vya majini wa TASAC Maulid Nsalamba na Gabriel Manase wakikagua chombo cha majini leo Novemba 13,2022 Ifakara, Mkoani Morogoro.
Afisa Masoko mwandamizi wa TASAC Martha Kelvin Akitoa maelekezo Kwa Baadhi ya wananchi namna ya kuvaa jaketi Okozi.
Afisa uhusiano mwandamizi wa TASAC Amina Miruko pamoja na Maafisa wa TASAC wakitoa elimu kwa mwananchi aliyejitokeza wakati wa zoezi hilo lililofanyika Ifakara, Morogoro.
(PICHA ZOTE NA: TASAC)
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa elimu ya ulinzi, usalama na utunzaji wa mazingira kwa wananchi mbalimbali katika wilaya ya Ifakara Mkoani Morogoro kwa lengo la kuwajengea uelewa wananchi hao katika maeneo hayo.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mafunzo hayo leo Novemba 13,2022, Afisa Ukaguzi na Mdhibiti wa vyombo vya majini wa TASAC Bw. Gabriel Manase amesema kuwa zoezi hilo lilianza Novemba 11, 2022 Ifakara Mkoani Morogoro na kwamba litaendelea katika mikoa mingine ya Iringa na Dodoma.
“Zoezi hili ni endelevu lilianza hapa Ifaraka Novemba 11, mwaka huu katika maeneo ya, Ngalimila, Ngapemba, Utengule, Chita, Mngeta na Mchombe, na linaendelea katika mikoa ya iringa na Dodoma” amesema Manase.
Shirika hilo limekuwa na desturi ya kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali yakiwemo ulinzi, usalama na utunzaji mazingira kwa wananchi wanaotumia vyombo vya majini pamoja na wale wanaofanya shughuli zao za kiuchumi majini kwa kuhakikisha wanapata uelewa wa kutosha ili elimu hiyo iwasaidie wanapokuwa kwenye majukumu yao ya kila siku wanapotumia vyombo vya usafiri majini.
Aidha, TASAC wameendesha zoezi la ukaguzi wa vyombo vya usafiri majini vinavyotumika katika eneo hilo.
Huo umekuwa ni muendelezo kwa TASAC kukutana na wananchi katika maeneo mbalimbali na kuwapa elimu kwa kuhakikisha kunakuwepo na ulinzi, usalama na utunzaji mazingira, katika maeneo yote ya bahari, maziwa, mito na mabwawa.
PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA MAFUNZO HAYO.