Home BUSINESS RAIS MWINYI AITAKA BENKI KUU KUWEZESHA DHAMANA ZA MIKOPO YA MIRADI YA...

RAIS MWINYI AITAKA BENKI KUU KUWEZESHA DHAMANA ZA MIKOPO YA MIRADI YA MAENDELEO ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuwezesha upatikanaji wa dhamana za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo Visiwani.

Dkt. Mwinyi ametoa maelekezo hayo alipokutana na Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania, Ikulu Zanzibar leo, chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Gavana wa BoT, Prof. Florens Luoga.

“Kwetu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar changamoto ni dhamana. Tunazungumza na taasisi mbalimbali za kifedha lakini huwa wanauliza tutadhamini vipi mikopo hiyo; na bila ya jibu hilo ina maana hatuwezi kupata fedha hizo na miradi yetu ya maendeleo inakwama kabisa,” alisema.

Rais Mwinyi aliongeza kuwa Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali imeonesha kuwa Serikali ya Mapinduzi inakopesheka, lakini haichukui mikopo kwa kiwango inachostahili kwa ajili ya miradi ya maendeleo kutokana na kukosekana kwa dhamana za mikopo hiyo.

“Wakati mwingine, miradi mikubwa sana kama ya reli ya kisasa (SGR) na mradi wa umeme katika Mto Rufiji tayari inajaza nafasi ya kukopa, na hiyo ni kwa upande mmoja. Je, tunaweza kufanya nini ili na Zanzibar ikawa na nafasi ya kukopa ili na upande mwingine tupate njia ya kuweza kupata fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo? Hilo ni jambo la msingi kama mkiliangalia,” alisema.

Aidha, Dkt. Mwinyi alisema kuwa katika mikopo ya nyumba iliyotolewa kwa Tanzania na Benki Kuu ya Dunia na kupelekwa katika benki za biashara kwa ajili ya kuwafikia wananchi kwa riba nafuu, Zanzibar bado haijafaidika. “Angalia namna ya kutusaidia moja kwa moja kupitia Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ili na sisi tuwe na njia nzuri ya kupata mikopo hiyo,” alishauri Rais huyo.

Dkt. Mwinyi ameipongeza BoT kwa kuendelea kusimamia vizuri uchumi wetu na ushauri inaotoa kwa Serikali zote mbili. “Hali ya uchumi wa Zanzibar baada ya Uviko-19 inaendelea kuimarika kutokana na kurejea kwa shughuli za utalii ambapo idadi ya watalii na mapato pia vinaongezeka,” alieleza.

Alisema kuwa vita vya Ukraine na Urusi vimechangia kupanda kwa bei za mafuta na chakula, na kuitaka Benki Kuu iendelee kusimamia na kukabiliana na hali hiyo ili kudhibiti mfumuko wa bei.

Mapema, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya BoT, Gavana Luoga alisema kuwa BoT ilichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na janga la Uviko-19, ikiwemo kuhakikisha uwepo wa ukwasi katika benki za biashara ambapo imesaidia kuimarisha uchumi wetu.

“Mwaka huu mwanzoni tulitegemea uchumi wetu utaendelea kukua kwa asilimia 4.8% lakini kutokana na ukame uliopo pengine tutaishia ukuaji wa asilimia 4.5%,” alisema. Prof. Luoga alisema kuwa Tanzania ndiyo nchi yenye viashiria vya Uchumi mpana vizuri Zaidi katika bara la Afrika ikilinganisha na nchi jirani ambapo hata mfumuko wa bei nchini umeendelea kuwa tulivu.

Gavana Luoga alisema kuwa ingawa katika kipindi hiki cha mgogoro wa Ukraine na Urusi bado uchumi wa Tanzania umekua vizuri, Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti mfumuko wa bei na kuhakikisha kuna utulivu wa bei nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here