Home Uncategorized KASI YA RAIS SAMIA YAWATOA WALIOKUWA PANGONI – SHAKA

KASI YA RAIS SAMIA YAWATOA WALIOKUWA PANGONI – SHAKA

-Asema utendaji wa Rais umefifiisha ndoto na matumaini ya wengi

-Asisitiza Chama kinaridhishwa na utendaji wa serikali, kinaunga mkono

Na MWANDISHI WETU, Babati

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka amesema kwa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan imewatoa nyoka pangoni kuja kuota jua la maendeleo.

Amesema kipaji cha uongozi cha Rais Samia ni chachu ya maendeleo endelevu, huku ubunifu wake ukileta ari mpya ya kusukuma maendeleo ya nchi.

Shaka amesema hayo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Babati mjini, ukiwa sehemu za shughuli za Rais Samia akikamilisha siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.

“Mheshimiwa Rais (Samia) na Watanzania msishangae kwa mambo makubwa yanayofanyika nyoka aliyoko pangoni atakuja juu, atakuja juu kutafuta jua ili akauke na kupata matumaini, mambo makubwa anayoyafanya Rais Samia Suluhu Hassan ameua ndoto, ameua matumaini ya watu…ndio imekwisha hiyo tena, tuombe uhai na uzima, tunaye (Rais Samia) kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu umoja wetu na mshikamano wetu habari 2030 penye uhai,” amesema huku akishangiliwa.

Shaka alisema Rais Samia ni kioo kinachoakisi utu na thamani ya Watanzania, huku kipaji chake cha siasa na uongozi imekuwa chachu ya maendeleo

Alieleza kuwa ubunifu wa Rais Samia umeleta ari mpya ya kusukuma maendeleo katka nchi, hivyo Watanzania waendelee kumuunga mkono.

“Ndugu zangu mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Rais Samia umeleta mageuzi makubwa katika nchi hii. Hatukuwa na mazoea kukaa kwenye mikutano hii…jamani nini mnachokitaka,” alisema.

Shaka alieleza kuwa Chama kinaridhishwa na kazi nzuri inayotekelezwa na Rais Samia katika kuwatumikia wananchi.

“Kwa Chama ni faraja na matumaini makubwa kwamba kumbe Rais wetu mambo yake si mabaya, mambo yake ni mazuri sana,”

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaridhishwa kabisa, nimewasikia mawaziri, nimewaona wananchi namna ambavyo mnapokea matumaini ya serikali yetu ambayo inaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Chama Cha Mapinduzi kinakutia moyo na kukutia nguvu mheshimiwa Rais, unakwenda vizuri wewe na timu yako endelea kuchapa kazi.

Hata hivyo, Shaka alisisitiza kuheshimiwa na kuenziwa kwa utamaduni wa kupongeza pale kiongozi anapofanya vizuri na kukosoa kwa heshima na staha pale mambo anapokuwa hayakwenda sawa.

“Tukajikumbusha utamaduni wa waafrika, pia tukajikumbusha utamaduni wa Watanzania tangu enzi za uhai wa baba wa taifa tangu enzi za uhai wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere utamaduni wetu Watanzania ukifanya vizuri unapongezwa, unapewa shukurani na unatiwa moyo ili ufanye vizuri zaidi, lakini utamaduni wetu pale ambapo hufanyi vizuri au mambo hayaendi vizuri Watanzania tumekuwa na utaratibu mzuri wa kukosoana kwa staha na heshima,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here