· Shangwe zaibuka baada ya kutangazwa mshindi
Na Mwandishi Wetu
Dk. Rose Rwakatare ameibuka na ushindi wa kishindo kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Mkoa wa Morogoro.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumamosi, msimamizi wa uchaguzi huo, Hassan Nyange, alisema kura zilizopigwa zilikuwa (722), zilizoharibika (45) na kura halali zilikuwa (677).
Kwenye uchaguzi huo, Dk. Rwakatare alipata kura (413), mgombea aliyeshika nafasi ya pili Yusuf kimwaga (156), Happy maswa (66) nafasi ya tatu na Milkel Mansuet (12) nafasi ya nne
Akizungumza mara baada kutangazwa mshindi, Dk. Rose alimshukuru Mungu kwa ushindi huo na aliwaasa wajumbe wa mkutano huo kumtanguliza Mungu mbele kwa kila jambo.
Aliwapongeza wajumbe wa mkutano huo kwa kumchangua kwa kishindo kwa kumpa kura nyingi.
“Nawashukuru sana kwa kweli leo hii nimejua kwamba wajumbe ni watu wazuri sana, nawashukuru wasimamizi wa uchaguzi umekwenda vizuri nachoomba tufanye kazi kwa pamoja tushirikiane kuinua jumuiya yetu isikike kama zilivyo jumuiya zingine,” alisema na kuongeza
“Mimi naahidi kuwa mwenyekiti wa dot.com tuwe na maendeleo ya 5G siyo maendeleo ya mwendo wa kinyonga nawaahidi kuwatumikia kwa upendo wa hali ya juu,” alisema
Akizungumza mara baada ya kutangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Hassan Nyange aliwataka walioshindwa wasikate tamaa na wasinune na badala yake wafanye kazi kwa ushirikiano na uongozi mpya wa jumuiya hiyo ili uweze kutimiza majukumu yao kwa ufasaha.
“Kura zikipungua unakubali matokeo na maisha yanaendelea kwa hiyo tukitoka hapa uchaguzi usiwe chanzo cha mifarakano na baada ya uchaguzi huu aliyeshinda ni jumuiya kwa hiyo msishangilie sana mkawakwanza wengine, sisi tunajuana kwenye chama chetu kwa hiyo msiharibu,” alisema