Home LOCAL UZINDUZI WA CHANJO YA UVIKO-19 AWAMU YA PILI MKOANI MOROGORO

UZINDUZI WA CHANJO YA UVIKO-19 AWAMU YA PILI MKOANI MOROGORO

Na. Hassan Kimweri – WAF, Morogoro

Wizara ya Afya kwa kutambua mchango wa jamii na viongozi wao katika kuongeza kasi ya utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 leo imezindua rasmi awamu ya pili ya kampeni hiyo Mkoani Morogoro.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mh. Alberto Msando wakati akizindua rasmi awamu ya pili ya utoaji wa huduma ya chanjo ya UVIKO-19 iliyofanyika katika viwanja vya Jamhuri Mkoa wa Morogoro.

“Sisi kama Serikali tumeruhusu wananchi wetu wachanje kwa hiyari kwa kuwa chanjo hii haina madhara yoyote katika mwili wa binadamu na mimi nimechanja na niko salama.” Amesema Mhe. Msando

Mhe. Msando amewatahadharisha wananchi kuacha tabia ya kubweteka kwakuwa wengine hawasikii habari za UVIKO-19 lakini ugonjwa huo upo tuendelee kuchukua tahadhari, pia tujitokeze kupata chanjo ya ugonjwa huo ili wote tuendelee kuwa salama.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kinga-Wizara ya Afya Dkt. Beatrice Mutayoba amesema kila chanjo zinapoingia nchini zinapimwa ili kujiridhisha na usalama wake kwakuwa chanjo hizo zinakwenda kutumika kwa watanzania.

“Hata tukikumbuka wakati wa uzinduzi wa awamu ya kwanza kwa utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alikuwa wa kwanza kupata chanjo hiyo hivyo chanjo hii ni salama.” Amesema Dkt. Mutayoba

Naye, Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Morogoro kwa kujitokeza kupata huduma hiyo ya chanjo kwakuwa tayari wamepata elimu na kujua chanjo hiyo ni Salama.

“Mimi nimechanja tarehe 24 Julai, 2021 na hadi sasa niko vizuri na hata nyumbani pia niko vizuri, chanjo hii haina madhara yeyote ni kama chanjo nyingine kwa kuwa lengo lake ni kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19.” Amesema Bw. Msigwa

Mwisho, Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Morogoro Bw. Masumbuko Ijembya amesema Mkoa huo ulianza rasmi kutoa chanjo ya UVIKO-19 Agosti 3, 2021 hadi kufikia Octoba 31, 2022 wamefikia asilimia 66.2 ya utoaji wa chanjo hiyo kwa wenye umri zaidi ya miaka 18.

“Leo hii tumefanya uzinduzi huu mkoani hapa kwa lengo la kuongeza kasi ya uchanjaji kwa kufikia zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wote wenye umri zaidi ya miaka 18 wawe wamepata chanjo ya UVIKO-19.” Amesema Bw. Masumbuko

Kampeni hii itaendelea katika mikoa saba mingine ambayo ni Pwani, Katavi, Rukwa, Manyara, Tanga, Simiyu na Singida na katika kila mkoa kampeni itaendeshwa katika kila halmashauri na kata zote ndani ya halmashauri husika, Lengo likiwa ni kusogeza zaidi huduma hii mahali alipo kila mwananchi.

“Bega kwa Bega, Ujanja Kuchanja”

#MtuNiAfya
#JaliAfyaYako

Previous articleBOCCO APIGA HAT-TRICK SIMBA IKIICHAPA RUVU SHOOTING 4-0
Next articleMAKAMU WA RAIS DKT.MPANGO ATAKA VIWANDA KUONGEZA UZALISHAJI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here