Home LOCAL WORLD VISION TANZANIA  YATOA VIFAA VYENYE THAMANI MILIONI 152 KWA SHULE ZA...

WORLD VISION TANZANIA  YATOA VIFAA VYENYE THAMANI MILIONI 152 KWA SHULE ZA MSINGI YA UYUI

Mkuu wa wilaya ya Uyui mkoani Tabora ,Kisare Makori akipokea moja ya dawati kutoka kwa Meneja wa World Vision Kanda ya Nzega,Jacqueline Kaihura kwa ajili ya kuzipatia shule za msingi katika vijiji vya Lutende,Mwisole,Itaga na Simbodamalu.

Meneja wa World Vision Kanda ya Nzega,Jacqueline Kaihura akitoa nasaha zake kwa jamii ya kata ya Lutende wilaya ya Uyui mkoa wa Tabora.

Mratibu wa Lutende AP, Michael Ngasa akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa Mpango kazi wa mwaka wa fedha 2021/2022 wa Mpango huo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Uyui,Kisare Makori.

Mkuu wa wilaya ya Uyui mkoani Tabora ,Kisare Makori akimkabidhi mtoto huyo kadi ya bima ya Afya iliyoboreshwa kwa ajili  ya matibabu.

Mkuu wa wilaya ya Uyui mkoani Tabora ,Kisare Makori akimkabishi mwanafunzi huyo wa shule ya msingi madaftari  na kulia kwake ni Meneja wa World Vision Kanda ya Nzega,Jacqueline Kaihura.

Na:: Lucas Raphael,Tabora

SHIRIKA la World Vision Tanzania kupitia wafadhili kutoka nchini ya Japan wametoa Madawati 590 , Madaftari 3200,Kalamu za wino 2500, Penseli 730 na sare 600 za wanafunzi, kwa wanafunzi wa shule za msingi vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 152.9 .

Akizungunza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo Mkuu wa wilaya ya Uyui,Kisare Makori alisema kuwa licha ya serikali kufanya kazi kubwa katika sekta ya elimu na afya lakini bado haijatosheleza hivyo kuwepo kwa wadau wa maendeleo kama vile shirika hilo ni muhimu sana kwa ustawi wa jamii .

Alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu imeweza kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita  hivyo ameitaka jamii kulinda miundo mbinu ya shule inayoletwa na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo kama vile shirika la World Vission ili iweze kusaidia watoto .

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu inafanya kazi kubwa sana katika nyanja zote ikiwemo ya elimu tumeshuhudia sasa elimu ya msingi hadi kudato cha sita kwa sasa inatolewa bila malipo na miundo mbinu inajengwa hivyo niwaombe wananchi tunzeni hii miundombinu iliyojengwa na serikali na ile iliyoletwa na wadau wetu wa maendeleo wakiwemo World Vision,”alisema Makori.

Naye Meneja wa World Visio Kanda ya Nzega,Jacqueline Kaihura alisema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo zenye lengo la kuibadilisha jamii katika kuboresha afya ya mtoto na mazingira ya kusoma na kujifunza katika shule za msingi.

Alisema kuwa wamebaini ya kuwa katika  kijiji cha Mwisole kuna changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama hivyo katika kipindi  cha utekelezaji wa Mpango huo moja ya kazi waliyopanga ni kuchimba kisima kirefu cha maji kitakachogharimu kiasi cha Shilingi 130 ili wananchi  waweze kupata maji safi na salama.

“Naishukuru Serikali ya Tanzania kwa kukubali sisi pamoja na wafadhili wetu wa Japan kuwa ni sehemu ya kuchochea maendelo kwa  wananchi wetu  hapa nchini natumaini kwa miaka 12 ijayo tutakayokuwepo kwenye eneo hili la Lutende nikuhaidi Mkuu wa wilaya tutafanya kazi kwa weledi mkubwa ili tuweze kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta zote ambazo tutazigusa hivyo wananchi waendelee kutupatia ushirikiano,”alisema Jacqueline.

Mratibu wa Lutende AP, Michael Ngasa   wakati akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa Mpango kazi wa mwaka wa fedha 2021/2022 wa Mpango huo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Uyui,Kisare Makori alisema kwamba wametoa kadi ya Bima za Afya iliyoborea  kwa  watoto 500 na vyeti vya kuzaliwa 208 kwa watoto waliozidi miaka mitano hasa wale waliotambuliwa kuwa na magonjwa sugu kama vile Selimundu ambao watapata fursa ya matibabu katika Hospitali za Rufaa kupitia uwezeshi wa shirika hilo sambamba na kutoa mafunzo ya lishe bora kwa watoto.

Alisema kuwa mradi huo ambao ni wa miaka 12 katika eneo hilo lenye vijiji vya Lutende,Mwisole,Itaga na Simbodamalu umepata mafanikio makubwa kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu ulipoanzishwa Oktoba 1 mwaka 2021 kutokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa serikali na wananchi wa eneo hilo.

Utoaji wa vifaa hivyo ni  utekelezaji wa shughuli za kuinua Ustawi wa Mtoto katika nyanja ya Elimu, Afya na Lishe, Maji, Usafi wa mazingira kupitia Mradi wa Mpango wa Maendeleo ya Jamii Lutende AP katika wilaya ya Uyui mkoa wa Tabora.

 Mwisho.

Previous articleWIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI YAITAKA BODI YA MPYA BARAZA LA TAIFA LA UJENZI KUTEKELEZA MAJUKUMU YENYE KULETA TIJA
Next articleTODAY’S NEWSPAPER FRONT PAGES ON FRIDAY 21st -2022
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here