WAZIRI wa Maliasili na Utalii Balozi Dk.Pindi Chana akizungumza alipokuwa akizundua mkutano wa Pili wa kuunganisha sekta ya tasnia na wasomi katika sekta ya utalii na ukarimu katika nchi zinazoendelea (LIATH) Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dk.Frolian Mtei akizungumza Katika mkutano huo.
Baadhi ya wadau wakifuatilia mkutano huo
Profesa Ndivhuwo Tshipala, kutoka Idara ya Usimamizi wa Utalii – Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Tshwane akizungumza.
Mkuu Wa Chuo cha Taifa cha Utalii ambaye sasa ni mbunge wa Afrika Mashariki Dkt. Queen Mlozi Sedoyeka akitoa mada katika mkutano huo.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Balozi Dk.Pindi Chana amesema kuwa ipo haja ya nchi zinazoendelea kujadili na kupanga namna bora ya kupiga hatua katika sekta ya utalii baada ya janga la UVIKO-19.
Balozi Dk.Chana ameyasema hayo alipokuwa akizundua mkutano wa Pili wa kuunganisha sekta ya tasnia na wasomi katika sekta ya utalii na ukarimu katika nchi zinazoendelea (LIATH), unaofanyika kwa siku mbili Oktoba 27 na 28, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa ni muhimu kwa wadau wote kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuendeleza Utalii katika Sekta ya Utalii.
“Nchi zinazoendelea kidogo zinahitaji kuja pamoja kujadili na kutoa jinsi zinavyoweza kuja pamoja baada ya uchumi kuathiriwa na janga la UVIKO-19.
“Tukio hili ni muhimu kwa sababu litakuwa jukwaa la nchi kujifunza uzoefu na masuluhisho ya kuokoa sekta ya utalii,” amesisitiza Dk.Chana.
Aidha Waziri huyo ameongeza kuwa, Tanzania kama nchi nyingine Duniani pia imeathiriwa na janga hilo na katika kujaribu kunusuru hali hiyo Serikali imechukua hatua kadhaa kama vile miongozo ya taratibu za kitaifa kwa watoa huduma katika mnyororo mzima wa Sekta ya Utalii.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dk.Frolian Mtei
amesema katika kongamano hilo jumla ya machapisho 55 yatawasilishwa kutoka katika nchi zilizoshiriki.
Amezitaja nchi zitakazowasilisha na idadi ya mawasilisho kwenye mabano ni Kenya (5), Afrika Kusini (15), Zambia (4), Namibia (3), Zimbabwe (6),Zanzibar (2) na zilizosalia zitawasilishwa na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT).
Wakati huo huo Profesa Ndivhuwo Tshipala, kutoka Idara ya Usimamizi wa Utalii – Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Tshwane amesisitiza haja ya nchi za Afrika kuimarisha soko lao la ndani.
“Tunahitaji kuendeleza, kusaidia na kukuza soko letu la kitalii la vijijini,” amesema.
Mkutano huo wa siku mbili utajidili mada mbalimbali zitakazolenga kuweka mkakati wa ustahimilivu na urejeshaji wa UVIKO-19 kwa utalii katika nchi zinazoendelea