Meneja wa TMDA kanda ya ziwa magharibi Dkt. Edgar Mahundi akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Madini yanayofanyika viwanja vya Bombambili EPZA Mkoani Geita.
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Meneja wa TMDA kanda ya ziwa magharibi Dkt. Edgar Mahundi (kulia) akitoa elimu kwa mwananchi aliyembelea Banda la Mamlaka hiyo katika Maonesho hayo.
Meneja wa TMDA kanda ya ziwa magharibi Dkt. Edgar Mahundi (katikati) akiwa pamoja na Afisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo Martin Malima (kushoto), na Mkaguzi msaidizi wa Dawa Kanda ya Ziwa Magharibi Gelard Uiso (kulia) wakiangalia Dawa zilizopigwa marufuku ambazo zimekamatwa na Mamlaka hiyo katika Maonesho ya Madini Geita.
Meneja wa TMDA kanda ya ziwa magharibi Dkt. Edgar Mahundi (katikati) akiwa pamoja na Afisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo Martin Malima (kushoto), na Mkaguzi msaidizi wa Dawa Kanda ya Ziwa Magharibi Gelard Uiso (kulia).
Muonekano wa Banda la TMDA katika Maonesho hayo.
GEITA.
Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya ziwa magharibi Dkt. Edgar Mahundi amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2021/22 mamlaka hiyo kanda ya ziwa magharibi, Geita imekamata Dawa mbalimbali zilizokwisha muda wa matumizi na zilizo chini ya kiwango, ambazo hazijasajiliwa zikiwemo dawa za kusisimua misuli na kuongeza nguvu za kiume ambazo ni feki.
Dkt. Mahundi ameyasema hayo leo Octoba 5, 2022 alipozungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya tano ya Sekta ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Bombambili EPZA Mkoani Geita.
Amesema kuwa Mamlaka hiyo imekuwa na kawaida ya kufanya ukaguzi katika maduka ya Dawa ili kubaini zilizokwisha muda wake na ambazo ni fei.
“Mamlaka ilifuatilia na kubaini uwepo wa Dawa nyingi za kuongeza nguvu za kiume na kusisimua misuli ambazo ni feki na kuziondoa ktika maduka hayo sambamba na kuwachukulia hatua za kisheria wa miliki wa maduka hayo” amesema Dkt. Mahundi.
Hata hivyo amewataka vijana wa kiume kuachana na matumizi ya dawa hizo za kuongeza nguvu za kiume kwani zina madhara makubwa yanayoweza kuchangia kuharibu mfumo wa uzazi.
Kuhusu kukamatwa kwa dawa za kuzuia kubeba ujauzito maarufu kama P2 ambazo ni feki na ambazo hazijasajiliwa hapa nchini Dkt Mahundi amesema kuwa walibaini dawa hizo zikiuzwa katika maduka ya kawaida ya dawa kinyume na utaratibu dawa hizo (zilizokidhi ubora) zinatakiwa zitolewe na madaktari katika vituo vya afya na si maduka ya dawa na tayari wamekwisha chukua hatua, huku akiwataka wanawake wanaotumia dawa hizo bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya waache mara moja kwani zinaweza kuchangia baadaye kushindwa kupata ujauzito endapo zitatumiwa bila kufuata ushauri wa wataalam wa afya.
Aidha mamlaka hiyo ya dawa na vifaa tiba imesema kuwa itaendelea na operesheni zake katika maeneo mbalimbali kukagua kama dawa na vifaa tiba vinavyouzwa madukani vimekidhi viwango vya ubora unaohitajika hapa nchini na itachukua hatua kwa wafanyabishara watakaobainika kuuza dawa hizo,sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya dawa,vifaa tiba na vitindanishi.
Kuhusu kushiriki katika Maonesho hayo Dkt. Mahundi amesema “lengo la mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba kanda ya ziwa magharibi, Geita kushiriki katika maonyesho haya ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya matumizi sahihi ya dawa,vifaa tiba na vitendanishi ili wananchi wawe na uelewa pindi wanapokwenda kununua Dawa hizo” amesema.