Home LOCAL UTEKELEZAJI WA DHANA YA AFYA MOJA WAANZA KWA KASI.

UTEKELEZAJI WA DHANA YA AFYA MOJA WAANZA KWA KASI.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Luteni Kanali Selestine Masalamado  akizungumza wakati wa ufunguzi  wa  warsha ya Uchambuzi wa Gharama na Manufaa ya Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja Nchini iliyofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma (kulia) kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Afya TAMISEMI, Bwa. Paul Chaote na (kushoto) ni Mratibu wa Mradi wa Homa ya Nguruwe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Dkt. Henry Magwisha.

Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu ) Makulu Butondo (Kulia) akifafanua jambo wakati wa kufunga warsha hiyo.

Mwenyekiti  Baraza la Utafiti kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dkt. Adrew Kitua akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungwa kwa warsha hiyo.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Na: Mwandishi Wetu -Dodoma

Sehemu ya Ufuatiliaji wa magonjwa yanayotoka kwa Wanyama kwenda kwa binadamu, inatarajiwa kuanza kazi baada ya kufanyiwa tathmini ya kina na wataalam wa magonjwa ya wanyama, kwa kushirikiana na wadau kutoka katika sekta ya Afya, Mifugo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).

Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu  Luteni Kanali Selestine Masalamado wakati wa ufunguzi  wa  warsha iliyofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma iliyolenga  kufanya Uchambuzi wa Gharama na Manufaa ya Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja Nchini.

Alisema kila sekta inapaswa kuwa na dhana ya afya katika sera za wizara husika hatua itakayosadia kupunguza madhara yanayotokana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu huku akihimiza elimu hiyo kufika  ngazi ya mamlaka ya Serikali za Mitaa.

“Ufanisi wa sehemu hii ukiboreshwa utasaidia kubanini na kushirikisha mapema wadau husika kuhsu uwepo wa viashiria vya magonjwa na majanga mengine ili kuchukua hatua za kuzuia na kudhibiti maafa kwa wakati,”Alisema Luteni Kanali Masalamado.

Pia aliwashukuru wataalam kwa kutoa suhirikiano wakati wa mjadala uliofanyika akisema umesaidia kupata elimu, kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabili magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Kwa upande wake Mwakilishi  kutoka Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) Dk .Henry Magwisa alieleza kwamba chombo hicho kinaenda na takwimu ambazo zitaingia katika maswali yatakayohusisha gharama za kufanya kazi kama timu badala ya kufanywa na sekta moja moja ili kupunguza gharama.

“ Baada ya kufanya uchambuzi wa kina tumeona chombo hiki kitatufaa  kwa sababu magonjwa ambayo yanashirikisha Wizara ya Afya na Wizara ya Mifugo kwa Tanzania ambayo yamepewa kipaumbele yapo sita, hivyo waliitwa wataalam wa sekta zote tatu kutoka sekta ya Mazingira, Mifugo na Afya ili kuchambua,”alisema Dk. Magwisa.

Aliyataja magonjwa sita yaliyowahi kufanyiwa kazi  kuwa ni pamoja na kichaa cha mbwa, homa ya bonde la ufa, homa ya mafua ya  ndege, ugonjwa wa kimeta, homa ya malale na kitupa mimba huku akisema, magonjwa hayo yote huwapata wanyama na binadamu.

Naye Mwenyekiti  Baraza la Utafiti kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dkt. Adrew Kitua alieleza kwamba kuna umuhimu wa kuimarisha mfumo wa namna ya kushirikiana katika afya, mazingira na wanyama katika kuzuia, kukinga na kujipanga namna ya kudhibiti madhara yanayotokana na magonjwa hayo.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here