Home BUSINESS KATIBU MKUU MADINI AWAALIKA WACHIMBAJI WADOGO KUSHIRIKI MAONESHO YA MADINI GEITA

KATIBU MKUU MADINI AWAALIKA WACHIMBAJI WADOGO KUSHIRIKI MAONESHO YA MADINI GEITA

*Zaidi ya Kampuni na Taasisi 600 zazimethibitisha kushiriki*

Katibu Mkuu Wizara ya Madini Adolf Ndunguru ametoa wito kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kushiriki Maonesho ya 5 ya Teknolojia ya Madini 2022 mkoani Geita kwa lengo la kujifunza namna bora ya utendaji wa shughuli zao.

Ndunguru amesema hayo baada ya kutembelea Maonesho hayo yaliyoanza leo Septemba 27, 2022 Mkoani Geita.

“Wizara ya Madini inayo mikakati mbalimbali ya kuwasaidia wachimbaji wadogo ili waweze kupata elimu ya uchimbaji madini na hatimaye waweze kuchimba kwa tija,” amesema Ndunguru.

Aidha, amesema Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wapo kwenye maonesho hayo kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo ili kupata taarifa sahihi ya uwepo wa madini katika maeneo yenye uchimbaji.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewapongeza waandaaji wa maonesho hayo na kuwataka kuzibainisha changamoto zilizojitokeza kwa lengo la kuboresha zaidi katika maenesho yatakayofuata ya mwaka 2023.

“Nimepata taarifa kwamba, zaidi ya kampuni na taasisi 800 zimealikwa kushiriki katika maonesho haya lakini kampuni 602 ndiyo zimethibitisha kushiriki hivyo, niuombe mkoa wa Geita na waandaaji wote kwa ujumla kuendelea kuyatangaza maonesho haya ili wadau wa madini wa ndani na nje ya nchi waweze kushiriki kwa wingi zaidi,” amesema Mbibo.

Pia, Mbibo amesema maonesho hayo yanalenga kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Sekta ya Madini kwa lengo la kuvutia wawekezaji ili kuchochea uchumi wa Taifa.

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Ndunguru ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Mbibo, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga na Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here