Home LOCAL KAMATI YA BUNGE YAISHAURI SERIKALI KUREJESHA USIMAMIZI WA MASUALA YA CHAKULA KWA...

KAMATI YA BUNGE YAISHAURI SERIKALI KUREJESHA USIMAMIZI WA MASUALA YA CHAKULA KWA TMDA

Na: WAF – Mwanza.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeishauri Serikali kufanya tathmini ya kina ya usimamizi wa masuala ya chakula kurejeshwa chini ya Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) ili kurahisisha utendaji kazi na kusimamia usalama wa chakula nchini.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Aloyce Kamamba (Mb) mara baada ya Kamati hiyo kufanya ziara katika Ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) Kanda ya Ziwa, Mwanza.

“Ni vyema Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara izikutanishe Kamati hizi mbili kukutana na kutoa ushauri ambao unakidhi mahitaji ya sasa huduma hizi kuwa sehemu moja” amesema Mhe. Kamamba na kuongezea kuwa masuala ya dawa na chakula kuwa haya ni maeneo yanayofanana ukichukua kwa upande wa chakula usimamizi uko TBS (Shirika la Viwango Tanzania) na dawa ziko TMDA.

Kwa upande wake Bw. Tumainieli Macha Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Mipango akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya amesema kuwa hadi Mwaka 2018 masuala ya usimamizi wa chakula yalikuwa chini ya TFDA (TMDA kwa sasa) kabla ya kuhamishiwa kwenda TBS.

Bw. Macha amesema Serikali imeanza kufanya mapitio upya ya usimamizi wa masuala ya chakula ili kuboresha upatikanaji wa huduma na kuongeza usimamizi wa masuala ya chakula na dawa nchini.

“Kulingana na tathmini itakayofanyika na kuwashirikisha wadau wote tutapata majibu na kuweza kuboresha huduma hizi kwa wananchi pasipo kupata madhara yeyote kwenye usimamizi wa chakula, dawa, vifaatiba au vipodozi” amesema Bw. Macha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here