Home LOCAL RAIS SAMIA KUWEZESHA USAFIRI WA WAJASIRIAMALI 250 KUSHIRIKI MAONESHO YA JUAKALI UGANDA

RAIS SAMIA KUWEZESHA USAFIRI WA WAJASIRIAMALI 250 KUSHIRIKI MAONESHO YA JUAKALI UGANDA

Mwenyekiti wa shirikisho la Vyama Vya Wajasiriamali Wadogo Tanzania Bw. Josephat Rweyemamu akichangia jambo wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Maonesho ya 22 ya Nguvu Kazi/Juakali yatakayo fanyika Kampala Uganda tarehe 08-18 Desemba 2022, jijini Dodoma tarehe 21 Septemba, 2022.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Maonesho ya 22 ya Nguvu Kazi/Juakali yatakayo fanyika Kampala Uganda tarehe 08-18 Desemba 2022, jijini Dodoma tarehe 21 Septemba, 2022.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan atawezesha usafiri wa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati 250 kushiriki Maonesho ya 22 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali yatakayofanyika Jijini Kampala, Uganda kuanzia tarehe 8 hadi 18 mwezi Desemba 2022.

“’Kipindi cha miaka mingi, pamoja na mambo mengine, serikali imekua ikichangia usafiri wa mizigo ya Wajasiriamali kwenda kwenye maonesho. Kwa mwaka huu, Serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Samia imepanga kuongeza mchango wake kwa kuwezesha usafiri wa basi la wajasiriamali kwenda na kurudi Uganda“

Mhe. Ndalichako amefafanua kuwa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itatumia maonesho hayo kwa lengo la kuwawezesha vijana wajasiriamali wa Tanzania kutumia fursa hiyo kutafuta masoko katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na  kuwawezesha vijana kujiajiri na hivyo kukuza ajira na kuondoa umaskini.

Akiongea na Waandishi wa habari jijijini Dodoma, tarehe 21 Septemba, 2022, Mhe. Waziri Ndalichako amesema Ofisi hiyo  kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwezeshaji – Zanzibar, Wizara, Taasisi nyingine za Serikali na Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali imejipanga kukahikisha inaibua vijana wajasiriamali mahiri wakiwemo watu wenye ulemavu watakaoiwakilisha Tanzania katika maonesho.

”Ninapenda kusisitiza kwa wahusika wote kuhakikisha wanawaibua na kuwateua vijana wajasiriamali kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.Maonesho haya hufanyika sambamba na mafunzo ya kuwajengea uwezo Wajasiriamali kuhusu masoko; Ubora wa bidhaa; Urasimishaji biashara; na Kuongeza  thamani ya bidhaa”

Kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu ni ”Nunua Bidhaa au Huduma za Afrika Mashariki ili Kuijenga Afrika Mashariki kwa Ustahimilivu na Maendeleo Endelevu”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Vya Wajasiriamali Wadogo Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Joseph Rweyemamu, ameshukuru kwa jitihada ambazo serikali imeendelea kuzifanya katika kuhakikisha wanashiriki maonesho hayo. Aidha, ameahidi kutangaza bidhaa za Tanzania, Utalii pamoja na lugha ya kiswahili.

Wajasiriamali wapatao 1,000 kutoka Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na Tanzania  ikiwa mojawapo watashiriki maonesho hayo.Aidha, wito umetolewa kwa Wajasiriamali wa Tanzania kujitokeza kushiriki maonesho.

Fomu za maombi pamoja na maelekezo kwa Wajasiriamali wanaokusudia kushiriki maonesho haya zitapatikana kuanzia tarehe 26 Septemba, 2022 katika Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa kote nchini na pia katika tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu: www.kazi.go.tz

Aidha, fomu hizo pia zitapatikana kupitia Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Wadogo ila zote zitapaswa kurudishwa kupitia Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa. Mwisho wa kurudisha fomu kupitia Halmashauri husika ni tarehe 17 Oktoba, 2022.

MWISHO.

Previous articleBUNGE LAPITISHA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI ZA FEDHA WA MWAKA 2022
Next articleNAIBU WAZIRI KIGAHE AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA AFRIKA KUWEKEZA TANZANIA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here