Home LOCAL HUDUMA JUMUISHI ZA TIBA ASILI NA TIBA ZA KISASA KUANZA KUTOLEWA NCHINI

HUDUMA JUMUISHI ZA TIBA ASILI NA TIBA ZA KISASA KUANZA KUTOLEWA NCHINI

Na:Catherine Sungura, Morogoro.

Serikali imeanza utoaji wa huduma jumuishi za tiba asili na tiba za kisasa katika vituo vya Momela Wilaya ya Meru mkoani Arusha na Maibong-SukiDar Magomeni katika jiji la Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Tiba Asili ya Mwafrika akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu yaliyofanyika Mkoani Morogoro.

Dkt.Kusirye amesema kuwa kuanzishwa kwa huduma hizo ni mafanikio makubwa kwani tangu UHURU wa nchi za kuboresha na kuendeleza huduma za tiba asili.

“Miongoni mwa mafanikio mengine ni tiba asili kutambuliwa katika Sera ya Afya,kutungwa kwa sheri ya Tiba Asili/Mbadala,kanuni na miongozo mbalimbali pamoja na kuongezeka kwa tafiti za tiba asili zinazofanywa na vyuo vikuu vya Serikali”Amesema.

Aidha, amesema mchango wa Tiba Asili umedhihirika zaidi wakati wa mapambano ya UVIKO-19 na kwamba viongozi na Serikali za Kiafrika zinawajibika kuona umuhimu wa kuboresha tiba hiyo katika mapambano ya adui maradhi.

“Huduma za tiba asili zilitumika wakati wa UVIKO-19 na zilifanya kazi kubwa sana kuwahudumia wahitaji ambapo dawa takribani 21 za asili zilitumika,kutokana na hilo Watanzania wamekuwa na imani kubwa na huduma za tiba asili”Aliongeza.

Hata hivyo amesema Tanzania suala la kuendeleza huduma za tiba asili ni mojawapo ya kipaumbele na moja ya vipaumbele katika Ilani ya CCM ambayo kwayo Serikali itapimwa.

Kwa upande mwingine amewataka Waganga wa Tiba Asili kutengeneza dawa zenye ubora na kuhakikiwa na Mamlaka zinazotambulika ikiwa pamoja na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuhusu usalama wa dawa zao.“Dawa zilizothibitishwa kuwa zina usalama kwa kiwango kinachokubalika ndizo zisajiliwe kwenye Baraza la TibaAsili/Mbadala”.

Pia amewataka Wanganga wa tiba asili kuacha kuchanganya dawa za kisasa kwenye dawa zinazotengenezwa na kuuzwa kwa wahitaji na kuongeza kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na taasisi za utafiti na vyuo inaendelea kufuatilia dawa zote za tiba asili zilizopo sokoni na dawa yoyote itakayokutwa imechanganywa na dawa za kisasa hatua kali zitachukuliwa kwa mmiliki wa dawa husika.

Naye, Mkurugenzi wa Uzamili na Utafiti kutoka SUA Prof. Esron Karimuribo amesema Tanzania ina mazao mazuri yanayofanya vizuri, yamethibitishwa ubora katika tiba na kuhakikiwa yanafanya vizuri.

Amesema SUA inaendelea kutoa elimu wa wataalamu wa tiba asili na kwa kuanza wamekuja na utaalamu wa vifungashio kwa dawa hizo pamoja na utoaji wa dozi kamili ili kupata matokeo mazuri.

Wakati huohuo Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Tiba Asili/Mbadala Bi. Elizabeth Lema amesema kutokana na kutatua changamoto za Baraza hilo hivi sasa wamewakamata vishoka na matapeli wanaopita kuwasajili waganga hao na hatua kali za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.

Bi.Lema amevihimiza vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuacha matangazo yasiyo na Vibali kutoka Baraza hilo na kwamba Baraza litaendelea kutoa elimu ili kuwa na wigo wa kuzidi kutoa tiba za Asili nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here