Home LOCAL TANZANIA NDIO NCHI PEKEE DUNIANI AMBAPO KOSA LA KASHFA KWA MWANAHABARI ...

TANZANIA NDIO NCHI PEKEE DUNIANI AMBAPO KOSA LA KASHFA KWA MWANAHABARI LINGEUZWA KUWA JINAI; MEENA

Ni kauli ya Neville Meena, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wakati akizungumza na Kituo cha Radio cha Dodoma (Dodoma FM) leo tarehe 18 Agosti 2022.

“Mpaka sasa Tanzania ndio nchi pekee duniani ambapo madai ya kashfa kwa mwanahabari yanageuzwa na kuwa kosa la jinai. Hili huwezi kulikuta kokote,’’ amesema.

Amesema, kashfa inapaswa kubaki kuwa madai kwa mwanahabari na sio kama ambavyo Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 inavyoelekeza.

Meena amesema, kuna lawama zinaelekezwa kwa vyombo vya habari kukosa weledi, moja ya changamoto inayovikabili ni kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati.

“Vyombo vya habari vinalalamikiwa kukosa weledi, lakini tukumbuke kwamba wanaotoa matangazo na kushindwa kulipa, wanachangia kutengeneza tatizo.

“Wanaoongoza kutolipa ni wakurugenzi wa halmashauri, hili linachangia kuyumbisha vyombo vya habari na ndio maana tumependekeza baada ya miezi sita mtangazaji kushindwa kulipa, licha ya kukumbushwa basi afikishwe mahakamani,’’ amesema.

Pia amesema, ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka wadau wa habari wakutane na kuchakata mapendekezo ya sheria za habari, imetimia.

“Suala la mapendekezo yote ya wadau wa habari kupita, hilo ni suala lingine. Cha msingi ni kwamba, miongoni mwa ahadi za Rais (Samia), ikiwemo wizara kukutana na wadau wa habari na kupitia vifungu, imetekelezwa.

“Sisi kama wadau wa habari tunaamini tunakwenda kufanikiwa kwa kuwa, hata Waziri Nape (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) ana hisia chanya katika mchakato huo,’’ amesema.

Amesema, miongoni mwa mapendekezo ya wadau wa habari katika mabadiliko ya sheria za habari nchini, ni kuwa uamuzi wa mahakama uwe unaheshimiwa.

Amesema, baadhi ya vyombo vya habari licha ya kushinda kesi mahakamani lakini kumaliza vifungo vyao, Idara ya Habari Malelezo iligoma kuwapa leseni ili kuendelea na upashaji habai.

“Kuna gazeti (MwanaHalisi) licha ya kushinda kesi mahakamani, hawakupewa leseni ya kuendelea na uchapaji habari. Hao hao pia hata walipomaza kifungo bado hawakupewa leseni, jambo hili sio sawa hata kidogo,’’ amesema Meena.

Amesema, wadau wa habari nchini wamependekeza kwamba, mahakama inapotoa hukumu juu ya jambo fulani, basi serikali inapaswa kutekeleza kinyume na ilivyo sasa.

“Mkurugenzi wa Habari Maelezo anatumia sheria ile ile ambayo sasa inalalamikiwa ya kuwa na uamuzi wa kutoa leseni kwa chombo cha habari ama kutotoa kwa utashi wake.

“Katika hili tunapendekeza gazeti likishasajiliwa basi liendelee na kazi kwa kufuata taratibu zilizopo. Unapofunga chombo cha habari ksiendelee na kazi, unakuwa umeathiri wengi ikiwemo wafanyakazi na hata wasomaji,’’ amesema Meena.

Pia amesema, wakati wa mabadiliko ya sheria zinazominya uhuru wa habari nchini ni sasa na kwamba, harakati za kudai mabadiliko ya sheria hizo ilianza siku moja baada ya sheria zilizopo sasa kusainiwa mwaka 2016 na kuanza kutumika.

“Awali serikali haikuonesha dhamira ya kushughulikua maoni ya wadau wa habari nchini, lakini katika utawala huu dhamira imeoneshwa tangu mwanzo, tunaamini tutafanikiwa,’’ amesema Meena.

Previous articleBASI LAUA WATANO SINGIDA AKIWAMO DIWANI WA CCM IRAMBA, HALMASHAURI YAMLILIA
Next articleKUTOKA MAGAZETINI IJUMAA YA LEO AGOSTI 19-2022
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here