Home LOCAL BASI LAUA WATANO SINGIDA AKIWAMO DIWANI WA CCM IRAMBA, HALMASHAURI YAMLILIA

BASI LAUA WATANO SINGIDA AKIWAMO DIWANI WA CCM IRAMBA, HALMASHAURI YAMLILIA

 

Na: Dotto Mwaibale, Singida

WATU watano wamefariki dunia akiwamo Diwani wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Tarafa ya Kinampanda wilayani Iramba mkoani hapa, Winjuka Mkumbo na wengine 15 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Tanzanite kupinduka.

Kufuatia kifo cha Diwani huyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi alisema halmashauri hiyo imempoteza mtu muhimu sana ambaye mwaka huu alikuwa ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango.

“Tumepokea  kwa masikitiko makubwa kifo cha diwani wetu huyu ambaye  alikuwa msaada mkubwa katika halmashauri na ni pigo kubwa kwetu tumuombee mwenzetu kwa Mwenyezi Mungu apumzike kwa amani” alisema Msengi.

Aidha Msengi lisema marehemu enzi za uhai wake alikuwa akitoa misaada mbalimbali kwa jamii na kutokana na utendaji kazi wake ulio tukuka na makini alimteua kuwa mjumbe wa kamati hiyo ya fedha na mipango ya halmashauri hiyo.

Msengi alisema Mkurugezi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba,  Michael Matomora tayari amekwenda mkoni Dodoma kwa ajili ya kuuchukua mwili wa diwani huyo. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa, amethibisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa ajali hiyo iliyohusisha basi namba  T 916 DNU  imetokea 9:30 alasiri katika Kijiji cha Mbwasa wilayani Manyoni Barabara
ya Singida-Dodoma.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Mwinjuka Mkumbo (40) ambaye ni Diwani wa Viti Maalum CCM wilaya ya Iramba, Alicia Flagence mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja
na wengine watatu ambao majina yao bado hawajambulika.

Diwani huyo alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya General mkoani Dodoma.

Kamanda Mutabihirwa alisema baada ya ajali majeruhi walikimbizwa katika hospitali ya General Dodoma kwa matibabu na baada ya uchunguzi majeruhi 11 waliruhusiwa baada kupatiwa matibabu na watatu wanaendelea na matibabu huku mmoja akipewa rufaa katika hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma.

Majeruhi wanaoendelea na matibabu ni Sharifati Mwipi (32) Rudia Kadila (59), Said Mbwana (39) na Abdul Ramadhani (32) ambao wanaendelea na matibabu
katika hospitali ya General Dodoma huku majeruhi mmoja Mwamba Sita (26) amepewa rufaa kwenda hospitali ya Benyamin Mkapa.

Alisema uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polish umebaini chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa basi hilo Abdul Kingwande ambaye alishindwa kulimudu kisha kuacha njia na kupinduka upande wa kulia wa barabara.

Kamanda Mutabihirwa alisema dereva wa basi hilo ambaye alitoroka baada ya ajali hiyo anatafutwa na jeshi la polisi.

“Jeshi la PolisiMkoa wa Singida linatoa wito kwa madereva wote wa vyombo vya usafiri kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali zisizokuwa na ulazima,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here