Home LOCAL TCU YATANGAZA KUFUNGULIWA KWA AWAMU YA PILI YA UDAHILI WA SHAHADA YA...

TCU YATANGAZA KUFUNGULIWA KWA AWAMU YA PILI YA UDAHILI WA SHAHADA YA KWANZA MWAKA WA MASOMO 2022/2023

Na: Hughes Dugilo, Dar es Salaam.

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kufunguliwa kwa Awamu ya pili ya udahili wa Shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2022/2023 kuanzia Agosti 24 hadi Septemba 6, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Agosti 24,2022 Jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Profesa Charles Kihampa amesema kuwa Dirisha hilo limefunguliwa ili kuendelea kutoa nafasi kwa wananfunzi wenye sifa kujiunga na Elimu ya Juu na kusisitiza kuwa waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakudahiliwa katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali kuitumia  fursa hiyo vizuri kwa kutuma maombi yao ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda.

Aidha Profesa Kihampa ameendelea kuwakumbusha waombaji wote wa udahili wa Shahada ya kwanza kuwa masuala yote yanayohusiana na udahili au kujithibitisha kwenye Chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika.

“Waombaji udahili wa Shahada ya kwanza wanakumbushwa kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika Chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika na kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa” Amesema Prof. Kihampa.

Pia Profesa Kihampa amesema kuwa TCU inawaasa wananchi wote kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri na kudai kutoa huduma ya kusaidia jinsi ya kujiunga na Vyuo vya Elimu ya Juu hapa nchini. 

Awali akitoa taafa ya udahili wa Awamu ya kwanza amesema kuwa jumla ya waombaji 106,295 wametuma maombi ya kujiunga katika vyuo 76 vilivyoidhinishwa kudahili.

Aidha jumla ya programu 757 zimeruhusiwa kudahili ikilinganishwa na programu 724 mwaka 2021/2022.

Ameongeza kuwa Kwa upande wa nafasi, mwaka huu kuna jumla ya nafasi 172,168 ikilinganishwa na nafasi 164,901 mwaka ukiopita ikiwa ni ongezeko la nafasi 7,267 sawa na asilimia 4.4

“Pia katika Awamu ya kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 75,163 sawa na asilimia 70.71 ya waombaji wote waliioomba udahili wameshapata udahili vyuoni” ameongeza Prof. Kihampa.

Previous articleMAKALA MAALUM : MZEE KINANA; HEKIMA , BUSARA NA MAARIFA YAKE YANAVYONOGESHA UIMARA WA CCM, SERIKALI
Next articleASKOFU MKUU WA KANISA ANGLIKANA ATOA WITO TANZANIA KUTUNZA MAZINGIRA KUEPUKA UKAME
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here