Home BUSINESS VIJANA NCHINI KUWEZESHWA UFUGAJI KIBIASHARA

VIJANA NCHINI KUWEZESHWA UFUGAJI KIBIASHARA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akiongea katika kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa na taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na taasisi inayojishughulisha na masuala ya kilimo biashara (PASS) katika kituo cha Kongwa kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022. Katika kikao hicho Mhe. Ulega alizitaka taasisi hizo kuhakikisha zinajikita katika vipaumbele vichache vinavyoweza kupimika na kuleta tija inayotarajiwa. Kushoto ni Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (sekta ya Mifugo), Dkt. Angelo Mwilawa 

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Sera na Mipango (sekta ya mifugo), Bw. Mbaraka Stambuli akifafanua jambo katika kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa na taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na taasisi inayojishughulisha na masuala ya kilimo biashara(PASS) katika kituo cha Kongwa kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022.

Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (sekta ya Mifugo), Dkt. Angelo Mwilawa (kushoto) akieleza kwa ufupi lengo la kikao  kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa na taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na taasisi inayojishughulisha na masuala ya kilimo biashara(PASS) katika kituo cha Kongwa kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022.

  Pichani ni Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa na taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na taasisi inayojishughulisha na masuala ya kilimo biashara (PASS) katika kituo cha Kongwa kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022. 

 

Na Mbaraka Kambona,

 

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ameitaka taasisi ya Utafiti wa Mifugo(TALIRI) na taasisi inayoshughulika na kilimo biashara(PASS) kupitia mradi wanaoutekeleza wa  kunenepesha mbuzi kuhakikisha vijana wengi wanapata ujuzi huo ili waweze kuwa na fursa pana ya ajira na kukuza uchumi wao.

Ulega alitoa maelekezo hayo katika kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa kwa ushirikiano na taasisi hizo mbili kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022.

Alisema mradi huo ni lazima ujikite katika kuwasaidia vijana wengi kupata ujuzi wa kufuga kibiashara na kuwawekea mfumo mzuri utakaowasaidia kuwezeshwa kifedha ili wawe na mitaji ya kutosha kuendesha biashara ya mifugo.

“Tunataka tutoe ajira kwa vijana, hivyo ni lazima kuwatengeneza vijana wengi watakaokuwa na ujuzi wa kunenepesha mifugo, sasa hivi wanaofanya unenepeshaji wapo na wanawezeshwa na benki zetu, lakini tunataka tupate vijana wengi zaidi watakaotengenezwa kupitia mradi huu, tukiweka nguvu yetu hapo vizuri naamini tutawezesha vijana wengi kujiajiri,”alisema.

Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa sasa sekta ya mifugo inakabiliwa na changamoto kubwa ya malisho  hivyo ni muhimu wakajikita katika kuzalisha malisho ili mifugo iwe na malisho ya kutosha wakati wote jambo litakalopelekea mifugo hiyo kuwa na uzito wenye thamani sokoni.

“Katika taarifa zenu nimewasikia hapa mmeeleza mambo mengi mnayotarajia kufanya kupitia mradi mnaotekeleza, ushauri wangu ni muhimu mkachagua mambo machache mtakayoweza kutekeleza vizuri awamu kwa awamu kuliko kubeba mambo mengi na mwisho wa siku msiweze kufikia malengo,” alisema Ulega.

Kufuatia changamoto ya kufa kwa mifugo iliyoikumba nchi hivi karibuni aliwataka wao kama Wataalamu kuhakikisha wanatumia taaluma zao kikamilifu ili kupunguza vifo vya mifugo nchini.

Halikadhalika aliitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kusaidia wadau hao wa sekta ya mifugo kwa kuandaa mipango mizuri ya biashara na kutoa mikopo nafuu kwa wafugaji ili waweze kufanya ufugaji wenye tija.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani, Dkt. Angelo Mwilawa alisema kuwa kwa muda sasa viwanda vingi vya kuchakata nyama hapa nchini vimekuwa vikifanya kazi chini ya uwezo wake hivyo kupitia mradi huo unaotekelezwa na TALIRI kwa kushirikiana na PASS ukisimamiwa vizuri utakwenda kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto hiyo.

Aliongeza kwa kusema kuwa mradi huo pia utashirikisha Halmashauri nchini ili vijana waliopo katika maeneo hayoo waweze kushirikishwa vizuri katika kujifunza unenepeshaji wa mifugo na kuboresha maisha yao.

Previous articleRAIS DKT. MWINYI AONGOZA MJADALA KUKUZA UWEKEZAJI WA MAKAMPUNI YA ULAYA NCHINI
Next articleBRELA, FCC, SIDO KUIMARISHA USHIRIKIANO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here