Home LOCAL UANDISHI WA HABARI NA CHANGAMOTO ZA KIDIGITI

UANDISHI WA HABARI NA CHANGAMOTO ZA KIDIGITI



Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka 2022 ilibebwa na kauli mbiu ya “Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti”. Msingi wa kauli mbiu hii ni kuibua mjadala juu ya namna waandishi na vyombo vya habari wanaweza kutatua changamoto na kutumia fursa zitokanazo na maendeleo ya kidigiti.

Ni ukweli kwamba maendeleo ya kidigiti hayakwepeki. Mwandishi Nielsen R. K. na wenzake katika chapisho lao “Changamoto na Fursa za vyombo na tasnia ya uandishi wa habari katika mazingira ya Kidigiti na Mitandao ya Kijamii” wameeleza jinsi mazingira ya uandishi wa habari yanavyobadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya kidigiti. Wanasema:

“Katika mazingira ya sasa, makampuni makubwa machache ya teknolojia yanawezesha mabilioni ya watumiaji duniani kuperuzi na kutumia vyombo vya kidigiti kwa njia rahisi na kuyavutia kupitia huduma kama kuperuzi, mitandao ya kijamii, kutumiana picha jongefu na ujumbe mbalimbali…Kwa wananchi, mazingira haya yanatoa fursa [na uhuru] ya chaguzi [ya vyanzo na njia za kubadilishana/kupeana taarifa]”.

Hata hivyo, matumizi ya teknolojia ya kidigiti yameleta changamoto mbalimbali katika tasnia hii na kuchagiza wanahabari kutafakari na kuweka mikakati ya kupata ufumbuzi wake. Kwa mujibu wa “Ripoti ya Muelekeo wa Dunia katika Uhuru wa Kujieleza” iliyotolewa na UNESCO mwaka 2021 takriban 50% ya magazeti ulimwenguni yamepoteza mapato yake kutokana na maendeleo ya kidigiti.

 Moja ya sababu ni matangazo mengi ya kibiashara kuelekezwa kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa ya mtandaoni yenye kuwafikia watu wengi kwa haraka na urahisi zaidi.

Aidha, magazeti yamepoteza wasomaji kutokana na ushindani wa mitandao ya kijamii inayorahisisha watumiaji kuwasiliana kupitia picha mgando na jongefu au ujumbe mfupi.

Pia, maendeleo ya kidigiti yamechangia mlipuko wa taarifa sehemu kubwa kati ya hizo ni taarifa za uongo, zinazopotosha umma, zinazochochea mmomonyoko wa maadili na tamaduni za Kitanzania.

 Mfano, mitandao ya kijamii imekuwa chanzo kikuu cha usambazaji wa taarifa za uongo na potofu kuhusu ugonjwa wa UVIKO 19 na chanjo zake. Taarifa hizi zimejenga na kuendeleza hali ya taharuki na hofu inayochangia wananchi kusuasua kupata chanjo ya ugonjwa huu hatari.

Sambamba na hilo, wadau wa habari bado hawajapata suluhisho kuhusu kuongezeka kwa uandishi wa kiraia (citizen journalism) mitandaoni kunakoambatana na kukosekana kwa uhakiki na uhariri wa maudhui yanayosambazwa. Uandishi wa kiraia ‘Citizen Journalism’ ni kitisho kwa tasnia ya uandishi wa habari kutokana na kutozingatia maadili na miongozo ya uandishi wa habari. 

Uwepo wa mfumo wa uhariri na uhakiki wa maudhui mtandaoni utasaidia kudhibiti usambazaji wa maudhui ya picha mnato na jongefu yanayohamasisha ngono, matumizi ya mihadharati, mauaji, wizi na tabia nyingine zisizofaa kwa jamii.

Kitisho kingine cha maendeleo ya kidigiti ni tishio la usalama kwa waandishi na vyombo vya habari wanaotumia vifaa na mifumo ya kidigiti katika kazi za uandishi wa habari. Vifaa na mifumo kidigiti ya udukuzi wa taarifa binafsi za waandishi, taarifa wanazozifuatilia na vyanzo vya taarifa ni tishio kwa usalama wa wanahabari na kazi ya uandishi wa habari.

 Bahati mbaya hakuna sheria zinazolinda usalama wa taarifa na faragha kwa waandishi na raia.

Kwa upande mwingine, maendeleo ya kidigiti yameongeza chachu ya ufanisi wa uandishi wa habari. Kazi za kiuandishi zimeimarika ikiwemo urahisi na uharaka wa kukusanya, kuchakata na kuripoti taarifa kwa kutumia vifaa na mifumo ya kidigiti.

 Pia, maendeleo ya kidigiti yanatoa fursa za kiuchumi kwa waandishi na vyombo vya habari vinavyozalisha na kusambaza taarifa zake kupitia majukwaa ya kihabari mitandaoni na mitandao ya kijamii. Hata hivyo, waandishi wengi nchini wamekosa weledi wa kuzitumia fursa hizi ili kujiimarisha kiuchumi.

Nini kifanyike?

👉Taasisi za kihabari zikiwemo MISA Tanzania, MCT na UTPC zishirikiane na wadau wa maendeleo kuendesha mafunzo endelevu nchi nzima ya usalama wa kidigiti wa waandishi na vyombo wa habari.

👉Vyombo na taasisi za kihabari zitoe elimu na uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuepuka kusambaza taarifa za uongo, potofu na zisizo na maadili.

👉Taasisi za kihabari ziendeshe mafunzo kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa kuzitumia fursa za kidigiti kujinufaisha kiuchumi.

👉Wadau wa habari kuhimiza utungwaji wa sheria itakayolinda faragha ya mtu na usalama wa taarifa binafsi za waandishi wa habari na vyanzo vyao vya taarifa dhidi ya udukuzi wa kidigiti.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here