Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 26,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu ajira hizo zilizotangazwa Aprili, Mwaka huu
Na:Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI imetangaza waombaji waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo katika kada ya Afya na Walimu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 26,2022 wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu ajira hizo zilizotangazwa Aprili, Mwaka huu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa.
Waziri Bashungwa,amesema kwa upande wa kada za Afya, Waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 6,876 wanawake ni 3,217 sawa na asilimia 46.8 na wanaume ni 3,659 sawa na asilimia 53.2 wakiwemo wenye ulemavu 42 sawa na asilimia 0.61
Aidha kutokana na uchache wa waombaji wenye sifa wa kundi hilo nafasi 736 kada za Afya zilikosa waombaji wenye sifa.
‘’ Kada hizo ni Daktari wa Meno 50, Tabibu Meno 43, Tabibu Msaidizi 244, Mteknolojia Mionzi 86 na Muuguzi- ngazi ya cheti 313. Kada hizi zitarudiwa kutangazwa ili kupata waombaji wenye sifa watakaojaza nafasi hizo’’amesema Waziri Bashungwa
Kwa upande wa kada za Ualimu, Waziri Bashungwa amesema kuwa waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 9,800 ambapo jumla ya walimu 5,000 wamepangwa shule za Msingi na walimu 4,800 Shule za sekondari, wakiwemo walimu wenye ulemavu wa shule za Msingi na Sekondari 261.
Amesema kuwa Kati ya Walimu 5,000 wa shule za Msingi wanawake ni 2,353 sawa na asilimia 47.06 na wanaume ni 2,647 sawa na asilimia 52.94,Kwa upande wa walimu 4,800 wa Shule za sekondari wanawake ni 1,289 sawa na asilimia 26.85 na wanaume ni 3,511 sawa na asilimia 73.15.
‘Walimu wenye ulemavu 261 wa shule za Msingi na Sekondari walioajiliwa ni sawa na asilimia 2.66 ya walimu wote walioajiliwa wakiwemo wanawake 84 na wanaume 177. Napenda ieleweke pia kuwa, kwa walimu wa sekondari tumetoa ajira za walimu wa sayansi kwa asilimia 76 ya nafasi 4,800 tulizopewa.”amesema
Waziri Bashungwa amesema kuwa hadi kufikia Mei 8, Mwaka huu maombi 165,948 yakiwamo ya wanawake 70,780 na wanaume 95,168 yaliyopokelewa kwenye mfumo, ambapo maombi ya kada za afya ni 42,558, na ualimu ni 123,390.
“Ili kufanikisha mchakato wa ajira, Ofisi ya Rais – TAMISEMI iliunda Timu Maalum, ya kufanya uchambuzi wa maombi ya ajira, iliyohusisha taasisi mbalimbali,”amesema.
Bashungwa amezitaja taasisi hizo kuwa ni Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Zingine ni Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi (NACTVET), Sekretarieti ya Ajira, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na Mabaraza ya Kitaalamu katika Sekta ya Afya.
Aidha Waziri Bashungwa amewaagiza waajiriwa wapya ambao hawataripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya siku 14, kuanzia leo watakuwa wamepoteza nafasi zao na zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa,waliopo kwenye Kanzidata ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
“Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo Waajiriwa wapya wamepangwa, wawapokee na kuwawezesha kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma, na baadaye kutoa taarifa ya kuripoti kwao,”amesema.
Hata hivyo amefafanua kuwa taarifa za kuripoti waajiriwa hao zijazwe kwenye mfumo wa kielektroniki (ajira.tamisemi.go.tz), baada ya kila mtumishi kupokelewa na kukamilisha taratibu.