Home BUSINESS MIKUTANO YA MPANGO WA SERA WA HUDUMA JUMUISHI BARANI AFRIKA (AFPI) KUFANYIKA...

MIKUTANO YA MPANGO WA SERA WA HUDUMA JUMUISHI BARANI AFRIKA (AFPI) KUFANYIKA ARUSHA

Benki Kuu ya Tanzania na Jumuiya ya kimataifa ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI) zimeandaa mkutano mkuu wa viongozi wa jumuiya hiyo ukanda wa Afrika (African Financial Inclusion Policy Initiative – AfPI) kuanzia tarehe 20 hadi 23 Juni jijini Arusha. Huu ni mkutano wa kwanza wa ana kwa ana kufanyika tangu kuzuka kwa janga la UVIKO-19. Katika mkutano huo, wanachama wa AFI barani Afrika wanajadiliana kuhusu “Umuhimu wa viongozi barani Afrika katika kuendeleza huduma jumuishi za fedha kwa njia ya kidigitali ili kuimarisha ukuaji wa uchumi’’
Magavana na manaibu gavana wa benki kuu barani Afrika watabadilishana uzoefu wa tatuzi za kisera zinachangia maendeleo ya huduma jumuishi za kifedha na namna ya kuondoa vikwazo katika kanda vinavyowakumba makundi maalumu kama wanawake, vijana wajasiriamali , wadogo na wa kati (MSMEs) na mengine
yaliyotengwa.


Huduma jumuishi za kifedha ni za muhimu na za lazima siyo tu kukuza huduma shirikishi za fedha, bali pia kusaidia kufikia malengo ya sera ya umma kuhusu uthabiti wa fedha na utulivu wa bei, Gavana Luoga alisema.


“Jinsi huduma za fedha zilivyo shirikishi miongoni mwa jamii na katika sekta zote, ndivyo ambavyo Benki Kuu na Serikali zinakuwa na ufanisi katika utekelezaji wa sera za maendeleo za Benki Kuu, “ alieleza Gavana Luoga.


Wakuu wa Taasisi za udhibiti na usimamizi wa sekta ya fedha pamoja na watunga sera kutoka taasisi wanachama zipatazo 32, zinazowakilisha nchi 30 wanashiriki katika mikutano ya wiki hii ya kubadilishana uzoefu na maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa sera za huduma jumuishi za fedha, kipaumbele kikiwa ni katika huduma za kidijiti za kifedha, uwezekano wa benki kuu kuanzisha fedha za kidijiti (CBDCs) ili kukuza huduma jumuishi za fedha na matumizi ya teknolojia katika usimamizi na udhibiti (SupTech & RegTech).


Pia watabadilishana uzoefu katika usimamizi wa teknolojia za kifedha (FInTechs), pamoja na huduma jumuishi za fedha kijinsia na kwa vijana. Wasemaji katika mkutano huu watakuwa viongozi kutoka Tanzania, Kenya, Mozambique, Eswatini, BCEAO, Ghana, Nigeria, na wengine. Mapema, mikutano ya Kundi la Wataalamu ya AfPI kuhusu Sera ya Huduma Jumuishi (EGFIP)Wataalam wa AfPI, na mafunzo kuhusu Udhibiti na Teknolojia za usimamizi na Mdahalo wa Sekta ya Umma na Binafsi na wa Nchi Zinazoendelea na Zilizoendelea iinafanyika. Aidha, kundi hili limechagua uongozi mpya ambapo Benki Kuu ya Namibia inachukua nafasi ya uenyekiti wa AfPI EGFIP kutoka Benki Kuu ya Morocco na Benki Kuu ya
Tanzania imechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kundi hilo.


“Kwa kupitia huduma za AFI ambazo zinalenga katika mafunzo-rika na kubadilishana ujuzi, pamonja na msaada wa kitaalamu, ushirikiano, na kujenga uwezo, wanachama wa AFI barani Afrika wametoa taarifa kwamba wamefanyia maboresho 150 ya kisera kati ya mwaka 2019 na 2021 katika maeneo makuu matatu : huduma za fedha za kidijiti, mkakati wa kitaifa wa huduma jumuishi na masuala ya fedha ya wajasiriamali wadogo na wa kati”, Mkurugenzi Mtendaji wa AFI, Dkt. Alfred Hannig anasema. 

Huduma za fedha za kidijiti, mkakati wa kitaifa wa huduma jumuishi na masuala ya fedha kwa wajasiriamali wadogo na wa kati yalikuwa maeneo muhimu ambayo nchi wanachama wa AFI zilitoa taarifa za mabadiliko ya kisera barani Afrika kwa mwaka 2021.


Bara la Afrka linachipukia katika ukuaji wa huduma za kidijiti, zikiongozwa na uunganishwaji wa kidijiti na upatikanaji wa simu za mkononi, ambazo zinaweza kuchangia ukuaji jumuishi na ubunifu wa huduma za fedha za kidigjiti na hivyo kuchangia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Hii ni kweli hasa kama
makundi yaliyo katika hatari kama wanawake, watu ambao wamehamishwa kwa nguvu kutoka katika makazi yao, au wanaoishi vijijini na sehemu za pembezoni. Ili kuhakikisha kwamba makundi hayo hayaachwi nyuma, mtandao wa AFI ulipitisha Kauli ya Kigali (Kigali Statement) kuhusu huduma jumuishi kwa makundi yaliyo
katika hatari wakati wa Mkutano wa Dunia wa Kisera (Global Policy Forum) uliofanyika nchini Rwanda.


“Huduma za kidigitali ni muhimu katika kuleta ufanisi wa huduma jumuishi za fedha na maendeleo kwa ujumla,” Gavana Luoga alisisitiza. Alieleza jinsi janga la UVIKO-19 lilivyokuwa mtihani mkubwa wa uhimilivu na utayari wa kukabili janga hilo ambalo lingeweza kukwamisha mifumo ya malipo nchini, pamoja na madhara mengine ambayo yangeweza kuathiri utulivu wa kifedha.


“Hatua za haraka za kisera za Benki Kuu kukabili janga hilo, ziliwezesha mifumo ya malipo kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi, watoa huduma za fedha kuendelea kufanya kazi bila mzigo mzito wa hatua za udhibiti wakati wote wa kipindi cha janga la UVIKO-19, na watumiaji wa huduma za kifedha waliweza kuendelea kufanya miamala pamoja na changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na janga hilo,” alieleza Gavana Luoga.


Katika kuongoza upatikanaji wa huduma endelevu na shirikishi za fedha kidijitali kupitia hatua za udhibiti, taasisi za usimamizi na udhibiti wa kifedha barani Afrika, zinahamasisha uundwaji wa mifumo inayoingiliana na ya malipo madogo, kipaumbele kikiwa mada zinazohusu fedha huria au fedha za kidijiti za benki kuu (CBDCs).


Kwa mfano, Benki Kuu ya Misri ilianzisha mfumo wa malipo ya papo kwa hapo (IPN) kuwezesha miamala ya fedha ya kielektroniki ya papo kwa hapo, huku Juni 2021 Benki Kuu ya Uganda ikianzisha rasmi usimamizi wa mazingira ya majaribio (regulatory sandbox) kwa mifumo ya kompyuta ambayo haijajaribiwa ili kuzisaidia taasisi za kiteknolojia za fedha (FinTechs) kuendeleza na kuanzisha bidhaa na huduma mpya. Wakati huo huo huduma za fedha kidijiti kama vile kupitia simu za mkononi zilikuwa na mchango mkubwa katika kupunguza umasikini kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha barani Afrika. Kutokana utafiti wa taasisi uliofanyika nchini Kenya, Uganda, na Tanzania, matumizi ya huduma za fedha kupitia simu za mkononi kwa kampuni za uzalishaji na huduma yalichangia kwa asilimia 16 uwezekano wa uwekezaji.


Wakati maendeleo ya huduma jumuishi na huduma pana za fedha kwa ujumla yanatarajiwa kuendelea kuamuliwa na maendeleo ya kidijitali, taasisi za udhibiti zinakabiliwa na maswali kadha yaliyo wazi, na ambayo yako nje ya mamlaka za benki kuu. Masuala haya ni pamoja na usalama wa kimtandani katika huduma za fedha kidijiti, wajibu wa usiri na utunzaji wa data katika kutoa huduma za kifedha, pamoja na elimu ya huduma za fedha kidijiti kwa walaji.


Jambo muhimu la kujifunza katika Mkutano huu wa 10 wa Viongozi ni Mpango wa sera wa kikanda kuhusu usimamizi teknolojia ya masuala ya fedha (FinTechs) barani Afrika, ambao utatoa mwongozo wa kitaalamu na kuweka vigezo kwa wadhibiti katika kanda wakati wanapotunga sera kwa ajili ya ukuajia FinTech. 

Katika ajenda pia kutakuwa na majadiliano kati ya sekta za umma na binafsi kuhusu hatua wezeshi zinazoweza kuchangia upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha kidijitali kitaifa na kikanda. Aidha, viongozi watamkaribisha Mwenyekiti Mpya wa AfPI, Bi. Caroline Abel, ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Ushelisheli pamoja na kumchagua Makamu Mwenyekiti mpya wa AfPI.


“Nimatazamio yatu kwamba, kuna haja ya kulinda maslahi ya Afrika katika mijadala ya dunia na kuhakikisha usawa katika mijadala na ushirikishwaji stahiki katika jukwaa la dunia”, Mkurugenzi Mtendaji wa AFI Dkt.


Hannig alisema. Alieleza kwamba kuendelea kuwasiliana na Bodi za Uwekaji Viwango (Standard Setting Bodies), kama vile FATFA, kutahakikisha kwamba viwango vinavyowekwa havififishi mafanikio yaliyopatikana katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha barani Afrika.


“Kanda hii ina nafasi pia ya kufaidika na majadiliano na watunga sera kutoka nchi zilizoendelea, ambayo yatawezesha upatikanaji wa faida kwa pande zote mbili na kuchangia michakato ya kisera kimataifa, kikanda na katika ngazi za kitaifa”, alihitimisha Dkt. Hannig.


Tangu kuanzishwa mwaka 2013, AfPI ni jukwaa la msingi la wanachama wa AFI barani Afrika kusaidia maendeleo ya sera za huduma jumuishi za fedha na mipango ya udhibiti, pamoja na kuratibu jitihada za mafunzo-rika. Ikiwa na makao yake makuu jijini Abidjan, Côte d’Ivoire, AfPI inawaleta pamoja wawakilishi wa

ngazi za juu kutoka watunga sera na taasisi za udhibiti barani Afrika ili kukuza utekelezaji wa sera na ubunifu wa huduma jumuishi za fedha barani Afrika.


Mikutano ya AfPI jijini Arusha imewezeshwa, pamoja na wengineMfuko wa Wadau wa AFI wa Utekelezaji wa Sera za Huduma Jumuishi, wakiwemo Shirika la Ushirikiano na Maendeleo la Ufaransa (AFD), Wizara ya Ushirikiano na Maendeleo ya Kiuchumi ya Jamhuri ya Ujerumani (BMZ) na Wizara ya Fedha ya Ufalme wa Luxembourg.


Kuhusu Benki Kuu ya Tanzania Benki Kuu ya Tanzania ilianishwa mwaka 1965 na kuanza kutoa huduma 1966. Makao Makuu ya Benki Kuu ni Dodoma. Jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha nchini ili
kuhakikisha kuna utulivu wa bei za ndani ili kuchangia ukuaji ndelevu wa uchumi wa taifa. Benki Kuu ya Tanzania ni mwanachama hao wa mtandao wa AFI, na tayari imeridhia ahadi 13 za Azimio la Maya, zikiwemo katika maeneo ya elimu ya fedha, wajasiriamali wadogo na wa kati na huduma za fedha kwa njia ya simu. Benki Kuu ya Tanzania pia ni moja ya Mabalozi wa AFI wa Ujumuishi wa Kijinsia, kutambua maendeleo muhimu yaliyochukuliwa na kutekeleza Mpango Kazi wa Denarau pamoja na kujitahidi kuunga mkono ushiriki mpana katika taasisi na kupunguza pengo la kijinsia katika kupata huduma jumuishi za fedha.


Kuhusu AFI.


AFI ni Jumuiya inayoongoza duniani katika masuala ya sera na udhibiti wa huduma jumuishi za fedha. Mtandao wa AFI unaundwa na takribani taasisi wanachama 100, zikiwemo benki kuu, wizara za fedha na mamlaka za udhibiti kutoka zaidi ya nchi 80 zinazoendelea na zinazoibukia. AFI inawawezesha watunga sera kuongeza upatikanaji na utumiaji wa huduma bora za fedha kwa watu ambao hawazipati kwa njia ya kutunga, kutekeleza na kuhamasisha kimataifa kuhusu sera endelevu na jumuifu.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here