Home LOCAL BRELA YAWASHIKA MKONO WATOTO YATIMA

BRELA YAWASHIKA MKONO WATOTO YATIMA

DAR ES SALAAM.

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), leo tarehe 18 Juni 2022 imetoa mahitaji katika Kituo cha Watoto Yatima Mwandaliwa, kilichopo Mbweni Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya mahitaji yaliyotolewa ni pamoja na mafuta ya kupikia, sabuni, unga wa sembe, mchele, maharage, madaftari, nguo,  dawa ya meno, penseli na  kalamu.

Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji kutoka BRELA, Bw. Daimon Kisyombe ameeleza kuwa lengo kubwa ni kuwatia moyo watoto  hao ili kuongeza juhudi ya kuzifuata ndoto zao.

BRELA ni taasisi ambayo inasimamia urasimishaji wa biashara, kwa miaka ijayo watoto hawa ndio tunatarajia washike hatamu katika uanzishwaji wa viwanda, ubunifu na biashara mbalimbali,” amefafanua Bw. Kisyombe na kuongeza  kuwa

mbegu inayopandwa ndani ya vijana hawa siku ya leo, inatarajiwa kuzaa matunda ambayo yatawanufaisha wao, jamii na taifa kwa ujumla.

Bi. Roida Andusamile ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kutoka BRELA, ameeleza kuwa katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma Taasisi itakutana pia na wadau wengine .

“Kuwashika mkono watoto hawa ni moja ya shughuli zitakazofanyika katika wiki hii, shughuli nyingine ni pamoja na huduma za papo kwa papo katika ofisi zetu zilizopo kwenye makutano ya Mtaa wa Shaaban Robert na barabara ya Sokoine, jijini Dar es Salaam,

kufanya usafi katika soko la Mbagala na pia Afisa Mtendaji Mkuu na Wakurugenzi  kukutana na wadau na kuwahudumia.

Katibu wa Kituo cha Watoto Yatima Mwandaliwa, Bw. Omari Abdul amesema kuwa ujio wa  BRELA kituoni hapo ni faraja kwao kama walezi  wa watoto hao. Pia wamepata fursa ya kujifunza kazi zinazofanywa na taasisi hiyo, elimu ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwao.

Mtoto Husna Issa anayelelewa katika kituo hicho, ameushukuru uongozi wa BRELA kwa kuwafikia na kuwapa usaidizi. Pia ametoa wito kwa taasisi binafsi na za umma kuwashika mkono ili waweze kuzifikia ndoto zao.

Wiki ya Utumishi wa umma kwa mwaka 2022 inaadhimishwa kuanzia tarehe 16 hadi 23 ya mwezi huu.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here