Mjane wa marehemu Lumba Amanzi kulia akipokea mkono wa pole( rambirambi) ya Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro aliyekwenda katika familia hiyo kufuatia kifo cha Mzee Lumba Amanzi aliyeuawa na Tembo.
Na: Muhidin Amri,Tunduru
MKAZI wa kijiji cha Marumba kata ya Marumba wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Lumba Amanzi, amefariki Dunia baada ya kujeruhiwa sehemu mbalimbali ya mwili wake na Tembo.
Tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki iliyopita,ambapo marehemu alipatwa na mkasa huo wakati akitoka shambani kuelekea kijijini kwa ajili ya kwenda kuswali swala wa Ijumaa.
Kwa mujibu wa mjukuu wa marehemu Said Halumba ni kwamba,marehemu alikuwa anaoga katika mto na ghafla alitokea Tembo mmoja aliyekwenda kwa ajili ya kunywa maji katika mto huo na kuanza kumshambulia.
Alisema, licha marehemu kujitahidi kukimbia kwa lengo la kuokoa maisha yake lakini alizidiwa mbio na Tembo huyo ambaye alimwangusha chini kumkanyaga sehemu mbalimbali na kufariki papo hapo.
Halumba ameishukuru Serikali kwa msaada uliotoa kwa ajili ya kufanikisha mazishi ya marehemu,hata hivyo ameiomba kupeleka askari wa Wanyamapori wengi kata ya Marumba ili kukabiliana na Tembo na wanyama wengine wakali na waharibifu.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Molandi kinachopakana na Marumba Mohamed Manjolo,ameiomba Serikali kupeleka askari katika kata ya Marumba ili kurudisha hali ya usalama kwani kama Tembo wataendelea kuachwa bila kudhibitiwa kuna hatari ya wananchi kushindwa kufanya shughuli zao za maendeleo kwa ofu ya kukutana na tembo.
Alisema,Tembo hao wanaotembea makundi makundi wanatoka katika Hifadhi ya Taifa ya Selou na mapori yaliyohifadhiwa kwa ajili ya uhifadhi wa misitu wamekuwa wakiharibu mazao mashambani na kuleta taharuki kubwa kwa wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro ambaye alifika nyumbani kwa marehemu kwa lengo la kuipa pole familia iliyompoteza mpendwa wao alisema,serikali imeshapeleka askari wa Wanyamapori ambao wameanza kazi ya kuwafukuza Tembo hao ili warudi katika maeneo yao.
Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Tunduru,amewataka wananchi wa kijiji hicho na maeneo mengine kuchukua tahadhari wanapokwenda shambani na kwenye shughuli nyingine pindi wanapoona dalili za kuwepo kwa wanyama wakali.
“tumetoka makao makuu ya wilaya kuja apa Marumba kwa ajili ya kushiriki pamoja nanyi majonzi haya makubwa mliyopitia kama familia ya kumpoteza mzee wa familia hii Lumba Amanzi,lakini mimi nilikuwa safari ya kikazi nje ya Tunduru lakini niliwatuma baadhi ya viongozi wengine kuja kushiriki kwenye msiba huu mkubwa”alisema.
Alisema, serikali ina wajibu wa kushiriki na kuwa bega kwa bega inapotokea misiba ya watu kuvamiwa na Tembo na wanyama wakali ambao wamekuwa tatizo kubwa katika maeneo yetu.
Alisema,kutokana na tatizo la watu kuvamiwa na kuuawa na wanyama wakali,serikali imeanza ujenzi wa kituo kikubwa cha askari wa wanyama pori ambao watakuja kwa ajili ya kukabiliana na wanyama hao.
Mtatiro,amemwagiza Afisa tarafa wa Nalasi na viongozi wa ngazi ya kata na kijiji kuhakikisha wanakuwa karibu na familia hiyo kwa lengo la kufahamu matatizo ikiwamo watoto kushindwa kwenda shule kwa kukosa sale na mahitaji mengine muhimu ili maisha yaweze kuendelea kama awali