Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana (kulia) akizungumza na wanafunzi wa fani ya mapokezi wa chuo hicho mara baada ya kufika Chuoni hapo na kuanza ziara ya kuangalia shughuli zinazofanywa katika sekta tofauti Chuoni hapo. PICHA NA: HUGHES DUGILO.
NA: MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM.
Katika kuhakikisha sekta ya Utalii hapa nchini inazidi kuimarika Serikali imesema kuwa ipo haja ya kuhakikisha kuwa Taasisi zake zilizopo kwenye sekta hiyo zinaimarishwa ili kuchochea maendeleo katika sekta hiyo.
hayo yameelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana leo Mei 19,2022 alipofanya ziara katika Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kilichopo Jijini Dar es Salaam ili kujionea shughuli mbalimbali zikiwemo za kitaaluma katika chuo hich.
Waziri Chana amesema kuwa Tanzania ni nchi inayofanya vizuri katika sekta ya utalii na kwamba Chuo hicho ni moja ya Taasisi muhimu zinazozalisha wataamu wa fani mbalimbali katika sekta hiyo hivyo wakati umefika wa kuwa na ubunifu kulingana na mahitaji ya soko.
Akizungumzia ‘Royal Tour’ Dkt. Chana amesema kuwa Filamu hiyo imeitangaza Tanzania na vivutio vya utalii vilivyopo nchini hivyo wadau wa sekta hiyo kutoka Serikalini na Sekta Binafsi wanapaswa kujipanga kikamilifu kupokea watalii wengi kutoka katika mataifa mbalimbali Duniani.
“Sekta ya utalii huchangia asilimia 17 kwenye Pato la Taifa (GDP), na imeajiri takribani watu mililioni 1.5 ajira za moja kwa moja,” alisema Chana, hivyo Filamu hii ya ‘Royal Tour’ inakwenda kufungua milango zaidi kwa kuleta wageni wengi kuja hapa nchini” amesema Dkt. Chana.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Dk. Shogo Mlozi Sedoyeka amemueleza Waziri huyo kuwa licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Taasisi hiyo ipo changamoto ya uhaba wa watumishi ususani wakufunzi na kwamba vipaumbele vya chuo hicho kwa mwaka wa fedha ujao ni kuimarisha mafunzo, kufanya utafiti, kutoa ushauri sekta ya utalii na kuanzishwa kwa sheria ya uendeshaji wa chuo, pamoja na kuongeza mapato,
“Chuo kilipata sh. bil 1.23 fedha za Uviko-19, zimesaidia kutoa mafunzo ya wadau 1,060 kwenye mikoa minane. Tunaomba kutoa changamoto kwako waziri mbali na mafanikio vyuo baadhi kuna uchakavu wa miundombinu.” amesema Dkt. Shogo.
Mwisho.