Home LOCAL WAZIRI BASHUNGWA AMALIZA MGOGORO WA ENEO ITAKAPOJENGWA HOSPITALI YA WILAYA MOSHI.

WAZIRI BASHUNGWA AMALIZA MGOGORO WA ENEO ITAKAPOJENGWA HOSPITALI YA WILAYA MOSHI.

KILIMANJARO.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amebariki mapendekezo ya Kamati ya Fedha, Uongozi  na Mipango  ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ya kujengwa kwa Hospitali ya Wilaya katika Kijiji cha Chekereni Kata ya  Mabogini mkoani Kilimanjaro.

Akikagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Waziri Bashungwa amesema Kamati ya Fedha , Uongozi na Mipango ikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi  tarehe 19 Agosti, 2021 walifanya maazimio kuwa hospitali ya wilaya ijengwe Kata ya Mabogini.

Waziri Bashungwa ameendelea kufafanua kuwa,  lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya hivyo kamati hiyo ipo sahihi  kulingana na miongozo iliyowekwa na Serikali.

Amesema, vigezo vilivyotumika kuchagua eneo hilo ni uwepo wa eneo ambalo halina mgogoro, wingi wa watu, jografia ya eneo, umbali wa eneo ambao ni kilomita 35 kutoka Moshi Mjini na uduni wa taasisi zilizopo katika Kata ya Mabogini tofauti na Kata ya Kilua Vyunjo Kusini ambapo mchakato wa kukabidhi ardhi kwa Mkurugenzi  bado unaendelea kwa kuwa bado wananchi hawajavuna mazao yao.

Amesema,Serikali ya Awamu ya Sita iliahidi kupeleka maendeleo nchi nzima bila ubaguzi  kwa kuwa wananchi wote wanahitaji kupata huduma bora za afya hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha anakamilisha mchakato wa kijiji kukabidhi ardhi na katika eneo hilo na kijengwe kituo cha afya katika Kata ya Kilua Vyunjo Kusini ili wananchi waweze kupata huduma za afya kwa karibu.

Waziri Bashungwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mhandisi Daniel Kileo  kuhakikisha anaanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya mara moja katika Kata ya Mabogini  na kumuagiza Meneja wa TARURA Mkoa  kuhakikisha wanajenga barabara katika eneo linalojengwa hospitali hiyo.

Aidha, mgogoro wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya umedumu kwa takribani miezi tisa  ambapo tayari kiasi cha shilingi milioni 500 zilishatengwa kwa ajili ya ujenzi huo katika bajeti ya mwaka 2021/2022.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here