Home LOCAL WABUNGE CHANGAMKIENI FURSA YA MAONESHO WIZARA YA NISHATI: WAZIRI MAKAMBA

WABUNGE CHANGAMKIENI FURSA YA MAONESHO WIZARA YA NISHATI: WAZIRI MAKAMBA

Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba leo Mei 23, 2022 amewaeleza wabunge kutumia fursa ya maonesho ya wizara ya nishati na taasisi zake ili kupata majibu ya changamoto zinazohusu utendaji wa Wizara na taasisi zilizo chini yake.

Akifungua maonesho hayo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Waziri Makamba amesema taasisi zote za wizara ya nishati pamoja na wakuu wa taasisi hizo watakuwepo katika viwanja hivyo kusikiliza na kutolea ufafanuzi mambo mbalimbali kwa wabunge kwenye maeneo yao ikiwemo masuala ya umeme.

“Kupitia maonesho haya wabunge watafahamu huduma zinazotolewa na Wizara ya nishati Pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo. Wabunge watafahamu na kupata majawabu ya maswali yao hapa kwa wakati mmoja,” amesema Waziri Makamba.

Kuhusu suala la ugumu wa upatikanaji wa taarifa Waziri Makamba amesema kuwa kupitia maonesho haya yatapunguza mlolongo wa upatikanaji wa taarifa na kupelekea urahisi wa kupata taarifa hizo.

“Kwa waheshimiwa wabunge muda wao wa kuchangia bungeni ni mchache na hawawezi kuchangia wote kwa wakati mmoja kwenye hotuba za bajeti na kwenye kuuliza maswali, tumeona nafasi hiyo waipate kwenye maonesho haya,” alifafanua Makamba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Maharage Chande amesema kuwa TANESCO inawakilishwa na mikoa ya KITANESCO 29, wilaya 132 na kanda 7 pamoja na uongozi mzima wa Shirika kwa lengo la kutoa majawabu ya changamoto kwa waheshimiwa wabunge.

“Tunaamini kupitia ushiriki wetu tunaweza kwa urahisi kufikisha taarifa kwa wateja wetu na wananchi kwa ujumla, vilevile waheshimiwa wabunge wanapokwenda kuzungumza na wananchi waweze kuwapatia taarifa sahihi na za uhakika za majawabu ya changamoto tulizokuwa nazo,” amesema Maharage.

Aidha akizungumzia hali ya upatikanaji wa umeme nchini Maharage amesema kwa sasa hakuna mgao wa umeme na Shirika limejipanga kuhakikisha umeme unakuwepo wa uhakika.

Haya ni maonesho ya kwanza ya aina yake kuandaliwa na Wizara ya nishati yakikutanisha taasisi zilizopo chini ya Wizara ya nishati pamoja na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maonesho hayo yatadumu kwa siku tatu na yanategemewa kumalizika tarehe 25 Mei,2022.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here