Home BUSINESS UMUHIMU WA KUSAJILI TOVUTI AU WAVUTI YAKO NA KIKAO CHA DOT TZ

UMUHIMU WA KUSAJILI TOVUTI AU WAVUTI YAKO NA KIKAO CHA DOT TZ

Kielelezo cha vikoa kwa nchi mbalimbali duniani; Tanzania ikionekana kwenye duara, ambapo utambulisho wa nchi ni kikoa cha .tz. Picha: Mtandao

Na: Mwandishi wetu.

Ni muhimu kusajili tovuti yako kwa kutumia kikoa cha dot tz (.tz) katika matumizi ya intaneti ili kutoa utambulisho wa kitaifa, na kukuza uchumi wa Taifa.

Kikoa cha dot tz (.tz) ni nini? ni rasilimali ya nchi (Tanzania) kwa ajili ya mawasiliano kwenye mtandao wa intaneti kupitia tovuti au barua pepe. Kila nchi imepewa utambulisho pekee mtandaoni.

Pamoja na jitihada ambazo zinafanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na hapo awali tzNIC bado kampuni nyingi na mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa na kufanya kazi Tanzania ni watumiaji wa vikoa vingine kama .com na .org.

Meneja Usimamizi wa Rasilimali za Mawasiliano na Teknolojia wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mwesigwa Felician akizungumzia umuhimu wa biashara na taasisi za serikali kusajili tovuti na utambulishi wa barua pepe zao kwa kikoa cha dot tz anasema kusajili tovuti au barua pepe kwa kutumia kikoa cha Tanzania kuna faida mbalimbali ikiwemo kupunguza gharama za mawasiliano, kuongeza wigo wa ulinzi wa taarifa na kukuza uchumi wa nchi kutokana na fedha zinazotumika kusajili vikoa hivyo kubaki nchini.

“Kwa wenzetu wanaotumia mtandao tunashauri wasajili majina yao kama vile tovuti na barua pepe kwa kikoa cha dot tz, kwa sababu vikoa vingine kama vile dot com haviwezi kuwa na msaada kwa Tanzania kwani fedha zinazotumika kusajili vikoa hivyo hupelekwa kwenye mataifa hayo ila ukijisajili kwa kikoa cha dot tz fedha zinabaki hapa nchini, usalama wa taarifa zako au taasisi yako unakuwa wa uhakika, na taarifa zako zinapatikana popote duniani, zaidi ya hayo jambo hili ni takwa la kisheria.” Alibainisha Mwesigwa.

Kila anwani ya mtandao, inacho kikoa kinachoishia, kinachojulikana pia kama kikoa cha ngazi ya juu cha nchi (country code top-level domain ccTLD).  Vikoa vya viwango vya juu vya msimbo wa nchi (ccTLDs) hutumika kuonyesha uhusiano wa tovuti na nchi au eneo mahususi (yaani .uk kwa Uingereza au .eu kwa Umoja wa Ulaya) na kwa hivyo hujulikana kama msimbo wa ki-nchi.

Mbali na kuwezesha fedha kubaki nchini suala ambalo linayo manufaa kwenye uchumi, Felician alisisitiza kuwa kikoa cha dot tz kinakupa utambulisho wa kitanzania katika Mtandao wa Intaneti; kinawezesha biashara yako kupatikana sehemu yoyote duniani kupitia mtandao wa Intaneti; aidha, matumizi ya kikoa cha .tz yanachangia kupunguza gharama za Mawasiliano kupitia Mtandao wa Intaneti.

“Kwa kweli faida za matumizi ya kikoa cha dot tz ni nyingi; mbali na hayo niliyoyaeleza hapo awali mengine ni pamoja na kikoa hiki kinatoa ushindani sawa wa kibiashara mtandaoni; kutoa au kuwezesha kipaumbele cha upatikanaji wa biashara zilizopo Tanzania mtandaoni hapa namaanisha yale mapendekezo biashara au huduma kieneo, mara nyingi mtandao utakuelekeza kwenye tovuti za nyumbani kwanza kabla hujafika huko kwingine, hii inakuwezesha kuwafikia wadau wako wa ndani ya nchi kwa urahisi zaidi” alibainisha na kuongeza.

Faida nyingine kwa mujibu wa afisa huyo wa TCRA ni kurahisisha utatuzi wa migogoro ihusuyo usajili wa majina chini ya kikoa cha.tz ambapo ni rahisi zaidi kutatua migogoro hiyo hapa nchini kwa sheria na kanuni za Tanzania, tofauti na majina ya kikoa yanayosajiliwa nchi nyingine au kimataifa; aidha kikoa cha .tz kinatoa uthibitisho thabiti wa bidhaa za kitanzania kwa wateja mtandaoni na kuongeza afua za usalama kwenye mtandao wa intaneti. Ni rahisi zaidi kudhibiti usalama wa huduma za kimtandao ikiwa tovuti imesajiliwa kwa jina la kikoa cha .tz

Usajili wa huduma za mtandao wa intaneti kwa kutumia kikoa cha .tz pia, unawezesha kuwasiliana, utoaji huduma, kurahisisha biashara kwa sekta ya umma na binafsi. Matumizi ya dot tz ni rahisi na panapotokea tatizo la kiufundi muhusika anapiga simu katika ofisi za TCRA na tatizo hutatuliwa papohapo tofauti na vikoa vingine ambavyo huhitaji kufuata mlolongo uliowekwa kwa ajili ya utatuzi wa tatizo husika ambao huchukua muda kutatuliwa.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here