Home BUSINESS TANESCO SHINYANGA YAHAMASISHA WANANCHI KUTUMIA MFUMO WA KIDIGITALI KUPATA HUDUMA ZA UMEME…YAANIKA...

TANESCO SHINYANGA YAHAMASISHA WANANCHI KUTUMIA MFUMO WA KIDIGITALI KUPATA HUDUMA ZA UMEME…YAANIKA FAIDA ZA ‘NIKONEKT’

Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Grace Ntungi akielezea kuhusu Mfumo rahisi wa maombi ya huduma ya Umeme kwa njia ya Mtandao ‘Kidigitali’ maarufu NIKONEKT ambao unamuwezesha mteja kupata huduma mbalimbali bila kufika katika ofisi za TANESCO leo Mei 31,2022 wakati wa Mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Shinyanga katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog.

Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Grace Ntungi akielezea kuhusu Mfumo rahisi wa maombi ya huduma ya Umeme kwa njia ya Mtandao ‘Kidigitali’ maarufu NIKONEKT ambao unamuwezesha mteja kupata huduma mbalimbali bila kufika katika ofisi za TANESCO leo Mei 31,2022 wakati wa Mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Shinyanga.

Na: Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewashauri wananchi kutumia Mfumo rahisi wa maombi ya huduma ya Umeme kwa njia ya Mtandao ‘Kidigitali’ maarufu NIKONEKT ambao unamuwezesha mteja kupata huduma mbalimbali bila kufika katika ofisi za TANESCO.

Ushauri huo umetolewa leo Jumatatu Mei 31,2022 na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Grace Ntungi kwenye Mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Shinyanga katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Mhandisi Ntungi amesema mfumo huo ni wa wazi, rahisi na unapunguza muda wa wateja kupata huduma ya umeme wakitumia muda mrefu kufuata huduma kwenye ofisi za TANESCO huku akiwaomba wananchi/wadau/wananchi kuwa tayari kuupokea mfumo huo kwa sababu ni mzuri kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wa Shinyanga na taifa kwa ujumla.

“Shirika la umeme Tanzania TANESCO limeendelea kuboresha upokeaji wa taarifa kutoka kwa wateja wake kwa kumrahisishia mteja kutoa taarifa. Tumekuja na bidhaa mpya ‘programu ya Nikonekt’. Mfumo huu wa Nikonekt unakuwezesha kutuma na kufuatilia maombi ya umeme kwa njia ya kidigitali, kutoa taarifa za dharura, kufanya maombi yasiyo ya umeme, kutoa malalamiko pamoja na kufanya maulizo mbalimbali. Huduma hii tayari imeshaanza kwenye baadhi ya mikoa na kwa upande wa mkoa wa Shinyanga huduma itaanza kabla ya mwisho wa mwezi Juni,2022”,ameeleza Mhandisi Ntungi.

“Lengo ya huduma hii ya Kidigitali ni kuhakikisha tunawapatia wateja wetu huduma ya umeme kwa haraka na wao wakiwa wanaendelea na shughuli zao
huko waliko, hauna sababu ya kufika ofisi za TANESCO kila kitu kitafanyika kwa njia ya digitali. Huduma hii inarahisisha sana kwa wafanyabiashara wanaohitaji huduma zetu.
Pia itapunguza manung’uniko mbalimbali na mianya ya rushwa na vishoka..Ukiomba maombi SMS itakuja, hatua tutakazokuwa tunazifanya SMS itakuja kwa hiyo utakuwa unajua kila hatua inayoendelea”,amesema

Akitoa elimu kuhusu Mfumo wa NIKONEKT, Afisa Mahusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Shinyanga Bi. Lilian Mungai amesema TANESCO inaenda kidigitali ambapo kupitia mfumo huo ,mteja/mwombaji wa huduma ya umeme anapaswa kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA) ili aweze kupata huduma ya maombi ya umeme kupitia mfumo wa Nikonekt.

“Mfumo huu unatumia njia kuu tatu kufanya kazi yaani maombi kupitia Kiswaswadu (USSD Code), Tovuti (Web portal) na Programu tumishi (Nikonekt Mobile App)”,amesema.
“Sasa mteja anaweza kutumia mfumo wa Nikonekt kwa kutumia njia ya Tovuti (Web portal) ya www.tanesco.co.tz ambapo mteja anaweza kutumia simu janja, komputa au kifaa kingine chenye uweo wa Intaneti. Njia nyingine inayotumika kupata mfumo wa Nikonekt ni kwa kutumia namba maalumu za USSD Code (Kiswaswadu) kwa kupiga namba *152*00# kwa watumiaji wa simu za kawaida.

Bonyeza *152*00#, nenda namba 4 (Nishati) kisha nenda tena namba 4 (TANESCO) baada ya hapo nenda namba 1 (Maombi ya umeme) baada ya hapo utaulizwa unahitaji kwa matumizi ya nyumbani/biashara/taasisi…Kila hatua unayofanya utakuwa unapatiwa Ujumbe (SMS) kwenye simu yako”,ameeleza Lilian.

Ameitaja njia nyingine ya kutumia mfumo wa Nikonekt ni kupitia Nikonekt Mobile App ambapo sasa unaweza kupakua Programu ya Nikonekt kwenye simu yenye uwezo wa Intaneti. App hii inapatikana kwa
watumiaji wote wa simu janja (Smartphone). Kwa watumiaji wa Android , Aplikesheni yetu ya Nikonekt inapatikana kwenye Play store na App store kwa watumiaji wa Iphone.
Amesema miongoni mwa faida za kutumia Nikonekt ni pamoja na kumrahisishia mteja kupata huduma kwa urahisi, inaokoa muda,inapunguza malalamiko ya kucheleweshewa huduma, urasimu, rushwa na mianya ya Vishoka na kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wateja waliopo maeneo ya pembezoni.

“Njia yoyote kati ya hizi yaani Kiswaswadu (USSD Code), Tovuti (Web portal) na Nikonekt Mobile App utakayotumia utafanikiwa kuunganishiwa umeme. Hatua zote zinafanyika kidigitali hadi kupata namba ya malipo na kulipia. Ni rahisi kufuatilia ombi lako la umeme limefikia wapi…kwa mawasiliano zaidi piga simu namba 0748 550 000 au tembelea tovuti yetu www.tanesco.co.tz”,ameongeza.

Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho akiwemo Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Shinyanga, Seif Hussein wameipongeza TANESCO kwa kuanzisha mfumo wa Nikonekt akieleza kuwa utasaidia kupunguza urasimu na vishoka “Tumekuwa tukiibiwa sana mfuko utasaidia kupunguza vishoka,naomba huduma ianze haraka”.

Afisa Mahusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Shinyanga Bi. Lilian Mungai akitoa elimu kuhusu Mfumo wa Nikonekt  kwa wafanyabiashara leo Mei 31,2022 wakati wa Mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Shinyanga. Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog.

Afisa Mahusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Shinyanga Bi. Lilian Mungai akielezea faida za Mfumo wa Nikonekt wakati wa Mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Shinyanga.

Afisa Mahusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Shinyanga Bi. Lilian Mungai akielezea faida za Mfumo wa Nikonekt wakati wa Mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Shinyanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here