Home LOCAL MAJI KUVING’ARISHA KIJIJI CHA STAHABU NA MIKUNGUNI WILAYANI PANGANI MKOA WA TANGA

MAJI KUVING’ARISHA KIJIJI CHA STAHABU NA MIKUNGUNI WILAYANI PANGANI MKOA WA TANGA

Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Pangani, Mhandisi Willybroad Mungereza akiwa na Mkandarasi wa Mradi wa Maji Mikinguni, John Msafiri kukagua hatua ya ujnzi ulipofikia.
Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, Ramadhan Hamad akielezea furaha aliyonayo kwa RUWASA kuwapelekea maji katika kijiji cha Stahabu.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Pendo Omary akielezea waandishi wa habari namna fedha za ustawi zinavyotekeleza miradi ya maji mkoani humo.
 

Muonekano wa nyumba ya kuweka pampu ya Mradi wa Maji Mikinguni wilayani Pangani mkoani Tanga.

Muonekano wa tenki la maji kwenye Mradi wa Maji Mikinguni wilayani Pangani mkoani Tanga.
 

Mwananchi wa kijiji cha Stahabu Wilaya ya Pangani Mkoa wa Tanga Mwanaidi Almas akielezea furaha aliyonayo baada ya RUWASA kuwapelekea mradi wa maji.

Mwenyekiti wa kijiji cha Stahabu kata ya Mikinguni Mussa Mzee akielezea furaha yao kwa kitendo cha RUWASA kuwapelekea mradi wa maji.
 
Na: Selemani Msuya, PANGANI.
WANANCHI wa Vijiji vya Stahabu na Mikunguni Wilaya ya Pangani Mkoa wa Tanga, wamesema mradi wa maji unatekelezwa kijijini kwao kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 utang’arisha vijiji hivyo.
 
Mradi huo unatekelezwa kwa zaidi ya Sh.milioni 533 fedha za mkopo usio na riba wa Sh.trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuomba ili kuhakikisha Sera ya Maji inayotaka kila mwananchi anachota maji kwa umbali wa mita 400.
 
Akizungumzia ujio wa mradi huo wa maji kijijini kwao, Mwana mama Mwanaidi Almas amesema wanatarajia kung’aa bada ya maji hayo kutoka kwani walikuwa wanatumia maji kwa kupima kutokana na changamoto ya upatikanaji.
 
“Hadi sasa hatujafungua koki maji yakatoka, ila imani yangu siku chache zijazo tutafungua koki, hivyo Shahabu itaanza kung’aa kama maeneo mengine yenye maji safi na salama,”amesema. 
 
amesema wamepitia mateso makubwa wakati wa kutafuta maji usiku wa manene kwa kuvamiwa na watu wabaya, huku wakiwa hawana amani pale ambapo wanaacha watoto wa kambo na waume zao ambao baadhi yao walikuwa wanashindwa kuvumilia.
 
Naye Mawazo Shaban amesema. “Sisi tumefurahi sana kwa kutuliwa ndoo kichwani kwani tumesulubika vya kutosha, naomba Rais Samia na Serikali yake waendelee kutumikia Watanzania,” amesema.
 
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilaya ya Pangani mkoa wa Tanga, Ramadhan Hamad (Diblo) amempongeza Rais Samia kuwaona Stahabu na kuweka bayana kuwa yoyote anayemuwazia mabaya kiongozi huyo Mwenyezi Mungu amuangamize.
 
“Mimi kama kiongozi wa CUF nitashirikiana na viongozi wa Serikali kuhakikisha mradi huu unalindwa ili uwe endelevu na kuing’anisha Stahabu na yoyote anayemtakia mabaya Rais Samia tunaomba asifanikiwe,” amesema.
 
Mwenyekiti wa kijiji cha Mikinguni, Kaoneka Jumaa amesema mradi huo utawaondolea adha ya kunywa maji ya madimbwi ambayo yalikuwa yanatumiwa pia na mifugo na wanyama kama nguruwe
 
Jumaa amesema pia changamoto ya maji Mikinguni ilikuwa inasababisha wanafunzi kuchelewa kwenda shule kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta maji.
 
“Mradi huu wa maji kata ya Mikinguni umekuja wakati muafaka kwani hitaji ni kubwa kwa wananchi wetu. Imani yangu ni ujio wa maji haya ubadilishe maisha yetu kuanzia usafi wa mazingira na maendeleo.
 
“Rais Samia ameupiga mwingi katika hili la maji, na Waziri wetu wa Maji Dogo Jumaa Aweso amecheza kama Simba. Tunawashukuru sana,” amesema.
 
Mwenyekiti wa kijiji cha Stahabu kata ya Mikinguni Mussa Mzee amesema wana zaidi ya miaka 35 ya kufuata maji kwa umbali wa kilometa tatu, hivyo ni imani yao kuwa wanaenda kufurahi maji bombani kama Watanzania wengine.“Tunamshukuru Rais Samia na RUWASA kwa kumtua ndoo mama kichwani, kwani amesaidia shughuli zingine kushika kasi,” amesema.
 
Mtendaji wa kijiji Stahabu Mwinyihamis Akida amesema mradi huu utachangia kumaliza migogoro kati ya wafugaji na wananchi kugombea maji kwenye madimbwi.
 
Akifafanua kuhusu mradi huo wa Maji Mikinguni, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Pangani, Mhandisi Willybroad Mungereza amesema mradi huo utanufaisha zaidi ya watu 4,990 vya vijiji vyote viwili.
 
Amesema wamejenga tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 135,000, kibanda cha pampu, mtandao wa kusambaza mabomba ya maji wenye urefu wa kilomita, vituo 21 katika vijiji vyote viwili na kinyoshea ng’ombe.
 
“Mradi huu unaotekelezwa na Kampuni ya NTU Business Network Limited, unagharimu zaidi ya Sh.533 utanufaisha zaidi ya watu 4,990 wa vijiji vya Mikinguni na Stahabu ambao wamekuwa wakiteseka kupata maji safi na salama. Lakini kukamilika kwa mradi huo kutaongeza asilimia ya upatikanaji maji wilayani Pangani hadi kufikia 70 kutoka asilimia 68 ya sasa,” amesema.
 
Akizungumzia miradi hiyo Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Pendo Omary amesema miradi ya maji mkoani hapo inagharimu zaidi ya Sh.bilioni 6.7 na itanufaisha wananchi 80,000.
 
Mhandisi Omary amesema zaidi ya vijiji 21 vitanufaika na fedha hizo katika majimbo 12 ya uchaguzi ya mkoa huo, hivyo lengo la mkoa kufikisha maji vijijini asilimia 85 na mijini asilimia 95 litatimia ifikapo 2025.
 
Mkandarasi wa mradi huo, John Msafiri amesema wamejipanga kumaliza mradi huo kwa wakati na ubora unaokubalika.
 
Amesema hadi sasa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 75 ya utekelezaji na kuiomba Serikali kuendelea kuwapa nafasi wakandarasi wazawa kutekeleza miradi.
 
Naye Fundi Geofrey Mnonganile amesema uamuzi wa Serikali kuwawapatia wakandarasi wazawa miradi mbalimbali utachochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa vijana.</p><p style=”text-align: center;”>Kwa upande wake Fundi Haji Abdallah ambaye pia ni Mkazi wa kijiji cha Stahabu amesema kupitia mradi huo amenufaika na kuiomba Serikali kuendelea kuwaletea miradi hiyo.
 
“Naujenga kwa nguvu zote kwa sababu ni mradi ambao unakuja kumaliza kero ya maji kijijini kwetu, tulikuwa tunafuata maji kijiji cha Sakura, Makarawe na Mtandu. Kusema kweli Rais Samia ametenda miujiza hapa kwetu,” amesema.

 

Previous articleYASEMAVYO MAGAZETI ASUBUHI YA LEO JUMAPILI MEI 1-2022
Next articleMWAMKO DUNI WA WAZAZI WAWAKOSESHA WATOTO CHAKULA SHULENI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here