Home ENTERTAINMENTS KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU YAELEZA MAFANIKIO ZIARA YA RAIS MAREKANI,...

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU YAELEZA MAFANIKIO ZIARA YA RAIS MAREKANI, ROYAL TOUR

 

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, leo Mei 12, 2022 imefafanua zaidi kuhusu mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan, nchini Marekani iliyojumuisha uzinduzi wa Filamu ya “Tanzania; The Royal Tour.” Mkutano huo pia ulihusu ziara ya Rais nchini Uganda juzi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Bi. Zuhura amesema ziara ya Rais nchini Marekani imekuwa na faida ambapo licha ya kukutana na wawekezaji wakubwa alishuhudia utiaji saini wa mikataba 7 kati ya makampuni ya Marekani na Tanzania yenye lengo la kufanya biashara na uwekezaji nchini ya zaidi ya shilingi Trilioni 11.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Balozi Liberata Mulamula amezungumzia ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Uganda hadi Tanzania na kusema kuwa kupitia ziara ya Rais nchini Uganda aliweza kufanya mkutano maalum na wadau wa sekta za mafuta na gesi kuhusina na ujenzi wa bomba hilo.

“Tulifanya mkutano maalum kuhusiana na ujenzi wa bomba hilo na mrejesho ni kwamba tayari hatua ya ulipaji fidia kwa wananchi imekamilika na sasa ujenzi wa bomba hilo utaanza mara moja”, alisema Balozi Mulamula.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Rais ya kuitangaza Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi, amesema Filamu ya Royal Tour imeonesha mafanikio makubwa sana na kwa sasa filamu hiyo imeendelea kusambazwa katika vituo vya televisheni karibu 300 kati ya 350 nchini Marekani na kwa hapa nchini tayari filamu hiyo imesambazwa katika vituo vyote vya televisheni.

“Filamu ya Royal Tour kwa sasa inapatikana katika mtandao wa Amazon na Apple tv, na takwimu zinaonesha kuwa filamu yetu imekuwa ikifuatiliwa zaidi kuliko Royal Tour nyingine zilizowahi kufanyika,”alisema Dkt. Abbasi.

Naye Katibu Mkuu  Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema filamu ya Royal Tour ina manufaa ya moja kwa moja katika Wizara hiyo kwani inatarajiwa kuleta wawekezaji, watalii na wafanyabiashara na wao kama Wizara wameandaa mkutano na wadau ili kupanga mikakati ya kuwekeza katika sekta ya utalii.

Naye mwakilishi wa Bodi ya Utalii (TTB) Amos Muko amesema kwa sasa bodi hiyo inatangaza kwa kasi vivutio vya utalii na hiyo inaenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya utalii ikiwemo barabara, usafiri na malazi.

 

Previous articleMADIWANI MKALAMA WATAKIWA KUSIMAMIA UKUSANYAJI MAPATO
Next articleKONGAMANO LA KUADHIMISHA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here