Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ya Waikizu ICDT Juma Makongoro (kushoto) akikabidhi kiasi cha shilingi Milioni 10 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bunda Changwa Mohamed kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Sanzate iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Bunda. Fedha hiyo imechangwa na kundi la ICDT kupitia kundi la mtandao wa kijamii Whatsapp. Picha na Frankius Cleophace.
Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ya Waikizu ICDT Juma Makongoro akionesha kiasi cha shilingi Milioni 10 kabla ya kukabidhi kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Sanzate iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Bunda fedha ambayo imechangwa na kundi la ICDT kupitia kundi la mtandao wa kijamii Whatssap.
Na: Frankius Cleophace – Bunda
Wanachama wa kundi la mtandao wa kijamii ‘Whatsapp Group’ maarufu ICDT ambalo linawaunganisha wazawa wa Ikizu wilaya ya Bunda Mkoani Mara kutoka maeneo mbalimbali nchini wamechangia shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Sanzate iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hizo Mei 9,2022 Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ya Waikizu ICDT Juma Makongoro amesema kuwa kupitia kundi la Whatsapp ambalo linaundwa wazawa wa Ikizu wilaya ya Bunda Mkoani Mara kutoka maeneo mbalimbali nchini wamechanga kiasi cha shilingi Milioni 10 kwa ajili ya kuunga nguvu za wananchi katika ujenzi wa shule mpya ya Sanzate.
“ICDT tunapongeza wananchi kwa kujitoa katika ujenzi huu naona mnaendelea na ujenzi na sisi tulipokutana kupitia Whatsapp Group yetu ya Wazawa wa Ikizu tulitoa ahadi ya kuchangia shilingi milioni 10 na leo kama mwakilishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ya Waikizu ICDT nimeleta hizo fedha kwa ajili ya kuwakabidhi”,alisema Makongoro.
Makongoro alieleza kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ya Waikizu ICDT umesajiliwa kisheria.
Makongoro alisisitiza fedha hizo na zingine zinazotolewa na wadau zisimamiwe vyema ili zilete matokeo chanya ili kuwaondoa wanafunzi katika changamoto ya kusafiri umbali mrefu kwenda shule na kuwaepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Makongoro aliiomba serikali kuweka mkono wake kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi ambao wameanzisha ujenzi tayari kwani wanafunzi wanatembea umbali mrefu jambo ambalo litaendelea kuchangia ufaulu kushuka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bunda Changwa Mohammed alisema Halmashauri itawaunga mkono wananchi hao katika ujenzi wa shule mpya ya Sanzate na kuagiza Afisa Elimu sekondari na Afisa tarafa ya Chamuriho kuhakikisha wanakutana na kijiji kimoja kinachodaiwa kugoma katika ujenzi huo ili kiweze kushiriki kikamilfu.
Vile vile Mkurugenzi aliwasisitiza wananchi kupeleka watoto wa kike shuleni ili kuweza kupata viongozi wa baadae licha ya shule kuwa mbali ambapo alisema kuwa katika Halmashauri ya Bunda bado kuna changamoto ya umbali wa shule.
Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ya Waikizu ICDT Juma Makongoro akionesha kiasi cha shilingi Milioni 10 kabla ya kukabidhi kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Sanzate iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Bunda. Fedha hiyo imechangwa na Wanakikundi wa kundi la Whatsapp la ICDT.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bunda Changwa Mohamed (kushoto) akikabidhi fedha kiasi cha shilingi Milioni 10 kwa mwenyekiti wa bodi ya ujenzi wa shule hiyo ambapo amesisitiza suala la kusimamia vyema ujenzi huo huku mapato na matumizi yakiwekwa wazi.
Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ya Waikizu ICDT Juma Makongoro akiongea na wananchi wa kijiji cha Sanzate ambapo amesisitiza mshikamano ili kuleta maendeleo kwa ajili ya kusaidia kizazi kijacho.
Hali ya ujenzi wa shule ya sekondari Mpya Sanzate iliyopo kata ya Mugeta inayojengwa kwa nguvu za wananchi ili kuwapunguzia wanafunzi umbali mrefu wanaotembea zaidi ya kilometa 20 kwenda na kurudi shule ya Sekondari Chamuriho.
Afisa elimu Sekondari Halmashauri ya wilaya ya Bunda Wandere Rwakatare akitoa ufafanuzi wa jambo katika kuboresha ujenzi wa madarasa yenye ubora.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilayaya Bunda Changwa Mohamed Mkwazu akishauri jambo katika ujenzi huo wa sekondari mpya ya Sanzate inayojengwa kwa nguvu za wananchi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Sanzate Adam Boniface akionesha hali halisi ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Sanzate.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Sanzate Oxygen Guti akisoma risala mbele ya mgeni rasmi na kueleza changamoto zinazowakabili ikiwemo suala la umbali mrefu ambao wanafunzi wanatembea na kuchagia baadhi yao kuacha shule na kushusha ufaulu kwa wanafunzi nakutumia fursa hiyo kuomba wadau kuendelea kujitokeza ili kuunga nguvu za wananchi.
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule ya Sanzate Godfey Mkata akitoa shukrani kwa wadau wa maendeleo kutoa kiasi cha shilingi Milioni 10 kwa ajili ya kuunga mkono nguvu za wananchi katika ujenzi huo.