Home LOCAL KATIBU MKUU CHONGOLO AELEKEZA VIONGOZI WOTE KUSHIRIKI VIKAO VYA MASHINA

KATIBU MKUU CHONGOLO AELEKEZA VIONGOZI WOTE KUSHIRIKI VIKAO VYA MASHINA

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo ametoa agizo kwa viongozi wa chama ngazi zote nchi nzima, kuanzia Tawi, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa kushiriki vikao vya mashina ili kuendelea kuimarisha zaidi CCM, ambacho msingi wa uimara wake unaanzia hapo.

Aidha, Ndugu Chongolo kasema kuwa, baada ya Uchaguzi Mkuu wa CCM unaoendelea nchi nzima, chama kitandaa mafunzo maalum kwa ajili ya viongozi wa chama ngazi zote nchi nzima kuanzia mabalozi mikoa hadi taifa ili wote wajue wajibu, ukubwa wa nafasi waliopewa, dhamana walizonazo, maadili na mambo ya msingi ya nafasi walizonazo.

“Nitumie nafasi hii kuhamasisha na kutoa agizo muhimu kwa ngazi zote za uongozi kuanzia tawi, kata, wilaya, mkoa mpaka taifa tushuke chini kwenda kuwatembelea na kushiriki vikao vya mashina vya mabalozi, tukishuka huku chini tukashiriki vikao vyao tutajua changamoto, na tukijua tutashiriki utatuzi wake.”

Katibu Mkuu ameyasema hayo leo tarehe 30 Mei, 2022 katika Mkutano wa Shina Namba 6, Tawi la Negezi, Kishapu mkoani Shinyanga katika ziara yake inayoendelea ikiwa na lengo la kukagua na kuhamasisha uhai wa chama pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aidha, kutokana na changamoto za baadhi ya miradi kuchelewa kukamilika kwa sababu ya uhaba wa fedha, Katibu Mkuu amezielekeza halmashauri kuacha kugawanya fedha katika miradi mingi na hivyo kushindwa kuikamilisha, badala yake, amezitaka zielekeze fedha katika miradi michache ya kipaumbele itakayotekelezwa kwa ukamilifu na kuleta matokeo yanayooneka na yenye tija kwa haraka

Katibu Mkuu ametoa maelekezo hayo wakati akikagua mradi wa daraja la Ipeja-Itilima wilayani Kishapu ambao umekamilika kwa gharama ya milioni 486.

“Sio mnapewa bilioni moja mnapeleka kwenye miradi 40, ambayo haikamiliki, hizo zama zimepita tunataka fedha zielekezwe kwenye mradi unaokwenda kukamilika kwa asilimia 100.

“Na sio fedha zitolewe kidogo kidogo zikafanye kazi kidogokidogo tija yake haionekani…hayo siyo mambo tunayotaka,” Katibu Mkuu Ndg. Chongolo amesisitiza

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu baada ya kupokea changamoto ya barabara ya Kolandoto – Meatu, ameahidi kusukuma upatikanaji wa fedha kutoka mfuko wa dharura kugharamia ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 53.

Previous articleUWEKEZAJI WA MIUNDOMBINU KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MAWENZI UTASAIDIA UPATIKANAJI WA HUDUMA BORA ZA MATIBABU
Next articleMAJALIWA AFUNGUA SEMINA YA WABUNGE KUHUSU SENSA YA WATU NA MAKAZI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here