Home BUSINESS BRELA YAKUSUDIA KUFUTA MAKAMPUNI 5,676

BRELA YAKUSUDIA KUFUTA MAKAMPUNI 5,676

DAR ES SALAAM.

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imekusudia kufuta Makampuni 5,576 ambayo yameshindwa kukidhi vigezo vya kisheria ikiwemo kutokuwasilisha Taarifa za Mwaka za Kampuni.

Hayo yamebainishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa katika mkutano na waandishi wa habari tarehe 27 Mei, 2022 katika ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi za taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam

Akifafanua kuhusu hatua hiyo Bw. Nyaisa amesema sheria ya Makampuni Sura 212 inazitaka kampuni zilizosajiliwa hapa nchini kuwasilisha taarifa za mwaka (Annual Return) ambapo kutofanya hivyo inatoa tafsiri kuwa kampuni haifanyi biashara kulingana na lengo la uanzishwaji wake.

Kwa upande wa kampuni za kigeni kifungu cha 438 sheria ya Makampuni kinazitaka Kampuni zilizosajiliwa nje ya nchi ambazo zina Ofisi za biashara hapa nchini kuwasilisha mizania ya mwaka (Financial Statement).

“Kutokana na hali hii vifungu vya 400 na 441 vya sheria ya makampuni vinanipa mamlaka kufuta kampuni ambazo haziwasilishi taarifa zake kwa msajili. Hivyo ninaanzisha mchakato wa kufuta kampuni ambazo hazifanyi biashara na haziwasilishi Taarifa za Mwaka na Mizania ya Mwaka katika Daftari la Makampuni” amesema Bw Nyaisa.

Aidha, Bw. Nyaisa ameeleza kuwa BRELA ilitoa taarifa ya zoezi hili kwa Taasisi ambazo tulibainisha kuwa zingeweza kwa namna moja au nyingine kuathirika kama vile Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Taasisi za Fedha

Amezitaja  sababu nyingine zinazofanya kampuni kuonekana hazifanyi biashara ni pamoja na, kukosa mtaji wa biashara, kuelemewa na migogoro baina ya wamiliki, kushindwa kutimiza malengo yaliyokusudiwa na hivyo kutokuwa na sababu ya kuendelea na uendeshaji wakampuni na kutokuwa na uelewa kuhusu wajibu wa Wakurugenzi na Wamiliki wa Kampuni.

Amewasihi wamiliki wa kampuni kutimiza wajibu wao ili taarifa zinazotakiwa na Msajili ziweze kuwasilishwa kwa wakati na wazingatie kila wanapo pata taarifa watekeleze kile ambacho sheria ya makampuni inawataka.

Katika awamu hii ya kwanza Taarifa itahusu makampuni yaliyosajiliwa nchini 5,284 na makampuni yaliyosajiliwa nje ya nchi 392. 

Orodha kamili ya makampuni haya inapatikana  kwenye Tovuti ya BRELA ambayo ni www.brela.go.tz.

 MWISHO .

Previous articleNABI, PABLO WATAMBIANA
Next articleTABORA KUANZA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA CT SCAN- PROF. MAKUBI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here