Home ENTERTAINMENTS SERIKALI KUWAPA BIMA WASHINDI WA TUZO ZA MUZIKI

SERIKALI KUWAPA BIMA WASHINDI WA TUZO ZA MUZIKI


Na. Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inawathamini wasanii ambapo itawakatia BIMA ya afya washindi wote wa Tuzo za mwaka 2021 kwa mwaka mzima ili kuwaondolea adha ya kupata matibabu wakiwa katika shughuli zao za muziki na nje ya muziki.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Mohamed Mchengerwa Aprili 2, 2022 wakati akifungua hafla ya kutoa tuzo za muziki 2021 jijini Dar es Salaam.
 

“Na hapa niseme tu, lengo la Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha wasanii, wanamichezo na wadau wa Sanaa wanawekewa mazingira mazuri ya ufanyajikazi na mazingira mazuri ya hapo baadae baada ya kustaafu kazi” amesema Waziri Mchengerwa.
 

Waziri Mchengerwa ameongeza kuwa pamoja na tuzo watakazopewa washindi na fedha kidogo za kujikimu, Serikali itatoa BIMA pamoja na pensheni kwa wale watakaoibuka kidedea katika tuzo zinazotolewa leo ili kuhakikisha wanakuwa na mazingira mazuri na salama wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
 

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema kuwa Serikali pia itawakatia pensheni wasanii wote ambao wataibuka kidedea na kuwa washindi na kuwalipia pensheni kwa mwaka mzima ikiwa ni mwanzo wa kuwaanzishia mfumo wa kujiwekea akiba uzeeni ili kuwaondolea adha ya kuwa ombaomba pindi kipindi chao cha kazi kinapofikia ukingoni. 
 

Tuzo za Muziki Tanzania 2021 zilizinduliwa Januari 8, 2022 jijini Dar es Salaam ambapo kazi za Sanaa1,360 ziliwasilishwa  kutoka kwa wasanii 500.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here