Na: Catherine Sungura,WAF-Dodoma
Serikali itahakikisha dawa na vifaa tiba za magonjwa yasiyoambukiza zinapatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe wakati wa kufunga mafunzo kwa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kwa watoa huduma za afya kutoka mikoa nane Tanzania bara yaliyofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Sichalwe amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imechua hatua mbalimbali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ya utekelezaji wa mkakati jumuishi wa III wa kuzuia na kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza 2021/2026.
“Mkatati huu unahuisha kuhakikisha watoa huduma wanapewa mafunzo ili waweze kutoa huduma bora za magonjwa yasiyoambukizwa kote nchini katika ngazi zote za utaji huduma za afya”.
Dkt. Sichalwe aliwataka washiriki hao kuwafundisha watoa huduma za afya waliopo katika mikoa wanayotoka ili kutimiza azma ya Serikali na hivyo kuchangia katika kuboresha nguvu kazi ya Taifa inayotegemea wananchi wenye afya njema.“Jitihada zozote zenye kusaidia mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukia zinaendelea kuungwa mkono na sisi wenyewe’ Alisisitiza.
Aidha, Mganga Mkuu wa Serikali aliwataka watoa huduma hao kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi wote ili watu wachukue tahadhari na kuepuka na magonjwa hayo au magonjwa hayo kutowaathiri zaidi na hivyo wanapaswa kuwashirikisha Viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji,kijiji,mtaa na kata.
Hata hivyo alitoa rai kwa wananchi kuacha tabia bwete na hivyo kuchuchua tahadhari ya kuepuka magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari,Moyo na mengine na kuhimiza kufanya mazoezi, kula mlo kamili na kuacha kutumia vileo kupita kiasi pamoja na kuacha matumizi ya tumbaku.
Dkt. Sichalwe ametoa rai kwa wadau wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa mafunzo mbalimbali katika sekta ya afya ili kuboresha huduma za afya na kukishukuru Chama cha Kisukari Tanzania(TDA) kwa kuwezesha mafunzo hayo kwa mikoa ya Kigoma, Lindi, Singida, Songwe, Arusha, kilimanjaro, Dodoma na Mara.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kuyoka Wizara ya Afya Dkt. Omary Ubuguyu amewakumbusha watoa huduma hao kuchukua historia ya mgonjwa anapofika kwenye kituo cha afya ili kuweza kutoa matibabu sahii.
-MWISHO-