Home BUSINESS SERA YA MIFUGO YACHOCHEA ONGEZEKO PATO LA TAIFA

SERA YA MIFUGO YACHOCHEA ONGEZEKO PATO LA TAIFA



Katibu Tawala (RAS) wa Mkoa wa Tabora Msalika Robert Makungu (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Shirika la Chakula Duniani (FAO) na washiriki wa mkutano wa mapitio ya Utekelezaji Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006, uliofanyika jana katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi mjini Tabora.

 Na: Lucas Raphael,Tabora

Kuwepo wa Sera ya Taifa ya Mifugonchini kumechocheo kikubwa kuboresha sekta ya mifugo na kuwezesha pato la taifa kuongezeka kutoka shilingi Trioni  1 mwaka 2006/2007 hadi tril 10.6 mwaka 2020/2021.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Msalika Makungu katika kikao cha mapitio ya utekelezaji sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 kilichohudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Idara za Mifugo kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na Katavi.

Alisema sera hiyo iliyoidhinishwa na kuanza kutumika nchini mwaka 2006 licha ya changamoto kadhaa imekuwa na tija kubwa kwa ukuaji wa sekta hiyo ikiwemo kutoa fursa kwa wadau wa mifugo kufanya shughuli zao.

Alibainisha mafanikio yaliyopatikana kupitia sera hiyo kuwa ni kuongezeka kwa mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la taifa kutoka wastani wa sh tril 1 mwaka 2006/07 hadi tril 10.6 mwaka 2020/21 kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya mwaka 2021 ambapo pato la taifa lilikuwa tril 148.5.

Faida nyingine ni ongezeko la mifugo kutoka ng’ombe mil 18.5 hadi 33.9, mbuzi kutoka mil 13.1 hadi mil 24.5, kondoo kutoka mil 3.5 hadi mil 8.5 na kuku kutoka mil 30 hadi mil 87.7.

Aidha idadi ya viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka 22 mwaka 2005/06 hadi 105 mwaka 2020/21, machinjio za kisasa kutoka 2 hadi 24, maabara 12 za kuchunguza magonjwa ya mifugo zilianzishwa na minada kuboreshwa.

Msalika aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 15 ya uwepo wa sera hiyo uwekezaji kwenye viwanda vya nyama umeongezeka kutoka kiwanda 1 hadi 11, majosho kutoka 1,860 hadi 2,763 na kujengwa kiwanda cha kuzalisha chanjo za mifugo ambacho sasa kinazalisha chanjo 7 badala ya 5 za awali.

‘Mafanikio haya yamechangia kuinua maisha ya wananchi kiuchumi, kuchangia upatikanaji malighafi katika viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya mifugo, kuinua biashara za mazao ya mifugo ndani na nje ya nchi na kuboresha lishe katika kaya’, alisema.

Alisisitiza kuwa sekta hiyo ingeweza kuwa na mchango mkubwa zaidi lakini uwepo wa changamoto kadhaa umechelewesha hatua hiyo, alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni uhaba wa miundombinu ya mifugo mfano majosho.

Nyingine ni koo za mifugo ya asili zenye tija ndogo katika uzalishaji mazao ya mifugo, kasi ndogo ya wafugaji kupokea na kutumia teknolojia bora za uzalishaji mifugo zinazoendana na wakati na kutokuwepo kwa ushirika wa wafugaji na wafanyabiashara.

Katibu Tawala aliongeza changamoto nyingine kuwa ni udhibiti hafifu wa magonjwa ya mifugo, uvamizi wa maeneo ya miundombinu ya mifugo, uhaba wa malisho ambao hupelekea kuhamahama na watoa huduma za pembejeo wasiokidhi ubora  na viwango vya kitaalamu.

Alishukuru serikali ya awamu ya 6 kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutoa maelekezo kwa Wizara za Kisekta kufanya mapitio ya sera zilizo chini yao angalau kila baada ya miaka 5 ili ziweze kuboreshwa na kwenda na mahitaji halisi ya jamii.

Alisisitiza kuwa kikao hicho ni muhimu sana kwani kitawapa fursa washiriki (kutoka sekta ya umma, binafsi na asasi za kiraia) kujadili na kutoa mapendekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa na serikali au sekta binafsi ili kumaliza changamoto za sera hiyo. 

Alitoa wito kwa washiriki wa kikao hicho kutoa ushirikiano unaotakiwa ilikufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kutoa mapendekezo yatakayowezesha sekta ya mifugo kuimarika zaidi na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Francis Ndumbaro aliwataka washiriki kutoa mapendekezo yenye tija ili sera hiyo iweze kuboreshwa kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Dkt John Laffa alisema sera hiyo imefafanua bayana malengo, mikakati, mwelekeo na mafanikio chanya yatakayopatikana na kubainisha kuwa kinachotakiwa ni usimamizi thabiti wa utekelezaji.

Kwa upande wake Ofisa wa Shirika hilo Moses Ole Neselle alisema kikao hicho kitasaidia kupata mrejesho wa wadau juu ya ufanisi wa sera hiyo, na kitu gani kifanyike ili kuboresha shughuli za wafugaji nchini na kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo.   

Mwisho.  

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here