Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Filamu ya Tanzania The Royal Tour uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Arusha International Conference Centre AICC Jijini Arusha tarehe 28, Aprili, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania Eliya Mjatta kuthamini mchango wake katika Tasnia hiyo mara baada ya uzinduzi wa Filamu ya Tanzania The Royal Tour Jijini Arusha 28, Aprili, 2022.
Viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Filamu ya Tanzania The Royal Tour uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Arusha International Conference Centre AICC Jijini Arusha tarehe 28, Aprili, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mwandishi wa Habari Maarufu wa Marekani ambaye ndiye mtayarishaji wa Filamu ya Tanzania The Royal Tour Peter Greenberg mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Mikutano wa Arusha International Conference Centre AICC Jijini Arusha kwa ajili ya uzinduzi wa Filamu hiyo tarehe 28, Aprili, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati akitoa misaada ya Vyakula mbalimbali pamoja na mafuta kwa vikundi 27 vya Watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi Mkoani Arusha tarehe 28, Aprili, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi mara baada ya kuwakabidhi msaada wa vyakula pamoja na mafuta kwa vituo mbalimbali 27 vya Watoto hao tarehe 28, Aprili, 2022.
Na: Happy Lazaro, Fullshangwe Blog – Arusha.
Arusha.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi filamu ya Tanzania Royal Tour leo mkoani Arusha huku akiwataka watanzania kuiunga mkono filamu hiyo kwani ni kwa faida yao na watanzania kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo Aprili 28,2022 Jijini Arusha wakati akizungumza filamu hiyo na wadau pamoja na wananchi mbalimbali katika uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa AICC uliopo mkoani Arusha.
Rais Samia amesema kuwa,filamu hiyo itasaidia kuchochea utalii kwa nchi yetu kwani baada ya kukamilika na kuanza kuonyeshwa katika nchi mbalimbali imeweza kuchochea utalii huku wengi wao wakitaka kuja kutembelea na kujionea vivutio mbalimbali.
Amewataka watanzania wote watakaopata fursa ya kujionea filamu hiyo kuwa mstari wa mbele kuisambaza ili iweze kuinufaisha nchi na kuwavutia watalii wengi zaidi.
“Katika uandaaji wa filamu hii nimekutana na changamoto nyingi Sana ikiwemo kutungiwa jina la Rambo na jina la Shoznigger kutokana na kuigiza filamu hiyo kwa kuwa nje ya ofisi siku nane kwa kutengeneza hiyo filamu huku nikiambiwa swala la urais niweke pembeni “amesema.
“Sijawahi kuandaa filamu ndo ugumu ulikuja hapo kutokana na kuwa nje siku nane na kuacha shughuli za utendaji wa urais halikuwa swala nyepesi kabisa ila namshukuru Mungu kwa kuwa tumefanikisha hilo.”amesema.
Amesema kuwa, anawashukuru Sana wafanyabiashara wa kitanzania kwa namna walivyojitolea kuchanga fedha kwa hiari yao wenyewe kwa ajili ya kufanikisha uandaaji wa filamu.
Rais Samia amesema kuwa, filamu hiyo italipa mara dufu kwa jinsi ilivyotengenezwa kwa umakini mkubwa na hiyo ni kwa maslahi ya nchi kwa sababu ni mara ya Kwanza kutengenezwa na gwiji maarufu wa Hollywood wa nchini Marekani.
Aidha katika filamu hiyo watanzania wataweza kujionea ghala la pembe za ndovu zilizopatikana kwa njia haramu na kuhifadhiwa kwenye ghala,ili watanzania waone jinsi wanyama wanavyouawa kikatili na kuona umuhimu wa kuhifadhi rasilimali hizo
Naye Muandaaji Mkuu wa filamu hiyo, Peter Greenberg amesema kuwa,anashukuru Sana kwa kupewa nafasi ya kutambuliwa na Rais katika kuandaa filamu hiyo na wameweza kufanikisha kwa siku nane.
“Tumepokelewa vizuri Sana na tumekuwa pamoja na Rais kwa muda wa siku nane na imekuwa ni changamoto Sana kwani kumwambia Rais awe muongozaji utalii sio kitu rahisi ,ila Rais ameweza kuwa nyota halisi katika filamu hii”amesema Peter.
Hata hivyo alimshukuru Rais kwa namna ambavyo amemwonyesha jinsi nchi yake ilivyo nzuri,huku akimshukuru kumteua yeye kuwa balozi wa kutangaza vivutio vya utalii katika nchi mbalimbali.
“Kwa kweli nampongeza sana Rais Samia kwa kufanya jambo hili kwani hakuna mtu yoyote aliyewahi kufanya Jambo hili kwa hapa Tanzania “amesema.