Home BUSINESS WADAU WAHIMIZWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU UTOAJI MAONI YA UBORESHAJI WA BIASHARA

WADAU WAHIMIZWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU UTOAJI MAONI YA UBORESHAJI WA BIASHARA

DODOMA.
SERIKALI yawahimiza wadau walioshiriki warsha ya maboresho ya matokeo ya awali ya utafiti wa mradi wa Biashara, Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub Project) kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni ya namna bora ya kuboresha biashara.

Hayo yamesemwa leo tarehe 28 Aprili, 2022 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe alipokuwa akizungumza na wadau walioshiriki warsha ya wadau kuhusu mradi wa Biashara, Maendeleo na Mazingira (Trade, Development and Environment – TRADE Hub Project) iliyofanyika katika ukumbi wa St. Gasper Dodoma.

Mhe. Kigahe akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Ashatu Kijaji Amesema kuwa mradi huu unatekelezwa katika kipindi muafaka ambacho nchi yetu inatekeleza sera ya kuinua uchumi kupitia uwekezaji katika sekta ya Viwanda na Biashara.
 
 


“Ni imani yangu kuwa katika kipindi cha miaka mitano ambapo mradi huu utakuwa unatekelezwa utasaidia kufungamanisha shughuli za biashara za bidhaa za kilimo, wanyamapori na sekta nyingine ili kuhakikisha kuwa biashara ya mazao haya yanakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi ambao ni shirikishi (inclusive economic growth) na kupunguza umasikini na kuleta maendeleo endelevu kama ilivyobainishwa katika malengo ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals) bila kusababisha ongezeko la uharibifu wa mazingira na upotevu wa bayoanuwai” Amesema Mhe. Kigahe.

Mhe. Kigahe amesema kuwa anaupongeza uongozi wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa mradi huu ambao unatekelezwa kwa kushirikiana na Washirika wa maendeleo kutoka nchi 15 za Afrika, Asia, Ulaya na Amerika ya Kusini na utasaidia kuongeza ubunifu katika mnyonyoro wa thamani na hatimae kuongeza kipato kwa wananchi na kuipatia serikali mapato.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Fulgence J. Mishili kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael T. Chibunda Amesema kuwa mradi wa (TRADE Hub) unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo kutoka nchi 15 za Afrika, Asia, Ulaya na Amerika ya Kusini.

Dkt. Mishili ameongeza kuwa Mradi huu unatekelezwa kwa muda wa miaka mitano (5) kuanzia mwezi Februari 2019 hadi Machi 2024, ukiwa na lengo la kufungamanisha shughuli za biashara za bidhaa za kilimo na wanyamapori ambapo Kwa Tanzania, mradi huu unafanya utafiti wa “Sera za Kibiashara na Matokeo ya Kiuchumi (Trade Policies and Economic Impact) kwa mazao ya Kahawa, Soya, Sukari na Wanyamapori.



 
Meneja Mkuu wa mradi wa (Trade HUB) Prof. Reuben Kadigi  Amesema kuwa utafiti huu unabainisha faida na hasara za kiuchumi, kimazingira na kijamii zinazotokana na utekelezaji wa sera hizi. Matokeo ya utafiti yanatarajiwa kutaarifu na kuwezesha kupatikana kwa sera na mikakati endelevu ya kibiashara ya bidhaa zinazofanyiwa utafiti ambapo lengo la warsha hiyo ni kuwasilisha matokeo ya awali ya utafiti wa mradi wa TRADE Hub kwa wadau na kupata maoni yao kuhusu changamoto hizo pamoja na mapendekezo ya kuzitatua.

Aidha, Mhe. Kigahe amepongeza wafadhili wa mradi huu ambao ni mfuko wa utafiti wa changamoto Duniani (The Global Challenges Research Fund – GCRF), Mfuko wa pamoja wa utafiti na Ubunifu wa Uingereza (UK Research and Innovation (UKRI) Collective Fund) kwa ufadhili na kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutafuta ufumbuzi wa kutatua changamoto zinazolenga kuboresha sera za kibiashara na uchumi ili kuleta tija na ufanisi kwa wananchi wetu wanaofanya shughuli za kilimo na biashara kwa mazao ya kilimo na wanyamapori.
Previous articleRAIS SAMIA AZINDUA RASMI FILAMU YA ROYAL TOUR MKOANI ARUSHA
Next articleWAZIRI UMMY AMUAGA MWAKILISHI MKAZI WA WHO ALIYEMALIZA MUDA WAKE NCHINI.
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here