Home Uncategorized MICHEZO WIZARA YA FEDHA BARA NA ZANZIBAR YAHAMASISHA UMOJA

MICHEZO WIZARA YA FEDHA BARA NA ZANZIBAR YAHAMASISHA UMOJA

Timu ya mpira wa pete kutoka Hazina Sport Club (walio vaa jezi nyekundu) na timu ya watumishi wa Chuo cha Mipango Dodoma, wakimenyana vikali katika viwanja vya Kilimani, jijini Dodoma ambapo Hazina iliibuka na goli 24 kwa 16.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Omolo, akiwataka wanamichezo kutoka Hazina Sport Club na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, kuitumia michezo kama chachu ya umoja, wakati akizungumza na wachezaji hao katika viwanja vya Kilimani, jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lusius Mwenda, akisalimiana na wachezaji wa mpira wa pete kutoka Hazina Sport Club, wakati wa michezo ya kipindi cha Pasaka kati yao na wanamichezo wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, katika Viwanja vya Kilimani, jijini Dodoma.


Timu ya wanaume ya mchezo wa kuvuta kamba kutoka Hazina Sport Club ambayo ilishinda dhidi ya timu ya wanamichezo kutoka Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar.


Timu ya wanaume ya mchezo wa kuvuta kamba kutoka Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar ambayo ilishindwa dhidi ya Hazina Sport Club, katika viwanja vya Kilimani, jijini Dodoma.


Timu ya wanawake ya mchezo wa kuvuta kamba kutoka Hazina Sport Club ambayo ilishinda dhidi ya timu ya wanamichezo kutoka Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar.


Timu ya wanawake ya mchezo wa kuvuta kamba kutoka Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar ambayo ilishindwa dhidi ya Hazina Sport Club, katika viwanja vya Kilimani, jijini Dodoma.


Kapteni wa Hazina Sport Club, Bw. Mgusi Msita, akimuhadaa mchezaji wa timu ya Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, katika viwanja vya Kilimani, jijini Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Omolo (katikati) Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Wizara hiyo Bw. Lusius Mwenda (walioketi kwenye viti wa pili kulia) na Mkuu wa Divisheni ya Utumishi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Bw. Hamza Mkuwi Hamza (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wanamichezo kutoka Ofisi hiyo, katika viwanja vya Kilimani, jijini Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Omolo (katikati) Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Wizara hiyo, Bw. Lusius Mwenda (walioketi kwenye viti wa pili kulia) na Mkuu wa Divisheni ya Utumishi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Bw. Hamza Mkuwi Hamza (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wanamichezo kutoka Hazina Sport Club, katika viwanja vya Kilimani, jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano, WFM, Dodoma)

Na. Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizaraya Fedha na Mipango Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Omolo, amewataka watumishi wa Wizara hiyo na watumishi wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, kuweka uzito unaostahili katika suala la michezo kwa kuwa linajenga umoja, udugu na afya ambayo ni chachu ya kutekeleza majukumu waliyopewa kwa ufanisi kwa manufaa ya Watanzania.

Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma wakati akizungumza na timu za wachezaji wa Hazina Sport Club kutoka Tanzania Bara na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango kutoka Zanzibar wakati wa michezo ya mpira wa miguu, pete na kuvuta kamba katika viwanja vya Kilimani, iliyolenga kujenga udugu na ushirikiano katika kulitumikia Taifa.

“Michezo inaleta afya, ushirikiano, uelewano na amani mambo ambayo ni muhimu katika kufanya vizuri katika maeneo yetu ya kazi, kutokana na umuhimu huo sisi watumishi wa wa Hazina tunalichukulia suala la michezo kwa umuhimu wa pekee”, alieleza Bi. Omolo.

Bi. Omolo aliwashukuru viongozi wa Hazina Sport club na wale wa Zanzibar kwa kushiriki michezo na akawataka kuendelea kufanya jitihada ya kufanya mazoezi hususani kwa timu ya mpira wa miguu ya Hazina Sport Club ambayo iliambulia kipigo cha magoli mawili kwa moja kutoka kwa wenzao wa Zanzibar.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Hazina Sport Club ambaye pia ni Kapteni wa timu hiyo, Bw. Mgusi Msita, alisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa na ushirikiano kati ya Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar na Bara katika masuala ya kikazi na kimichezo, ambapo katika michezo kwa kipindi hiki Wizara ya Fedha na Mipango Bara ndio wenyeji wa michezo hiyo ya tamasha la Pasaka na mwakani Zanzibar watakuwa wenyeji.

“Hii michezo ina umuhimu mkubwa kwetu kama watumishi wa umma, kwa kuwa tunajenga mahusiano nje ya kazi na ndani ya kazi lakini pia michezo hii inalenga kuboresha afya ya wafanyakazi kwa kuwa tunatumia muda mwingi kwa kazi za ofisini, hivyo tunapopata fursa kama hizi, akili na mwili unachangamka”, alieleza Bw. Msita.

Alisema kuwa lengo la michezo hiyo sio ushindani wa kutafuta pointi tatu bali kudumisha umoja na mshikamano. Aidha tamasha hilo la michezo la kipindi cha  Pasaka ni mwendelezo wa michezo ya Mei Mosi.

Bw. Msita alikiri kuwa wachezaji upande wa mpira wa miguu kutoka Zanzibar walikuwa bora kuliko bara hivyo watajipanga vizuri kwa awamu ijayo lakini alibainisha kuwa wachezaji hao ni fursa kwa timu ya Wizara ya Fedha na Mipango katika mashindano ya Mei Mosi kwa kuwa wanaandaa timu moja dhidi ya timu zingine zitakazoshiriki.

Kwa upande wake Kapteni wa timu kutoka Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Bw. Hamza Mkuwi Hamza, alisema kuwa kwa ujumla michezo ina faida nyingi ikiwemo ya kukuza upeo wa mambo na kuendeleza udugu ambao umeasisiwa na Serikali zote mbili na wao wanaendeleza katika muktadha wa michezo.

“Tumeshindana, upande wa Zanzibar tumepata ushindi kwenye mpira wa miguu ambapo tumeshinda mbili kwa moja na upande wa kuvuta kamba tunawapongeza wenzetu wa Bara kwa kuchukua ushindi kwa timu ya wanawake na wanaume.

Naye Kapteni wa timu ya mpira wa pete ya Hazina Sport Club, Bi. Eva Masasi, aliwashukuru viongozi wa Wizara hiyo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa kutoa nafasi ya michezo ambayo inasaidia pia kuweka mahusiano mazuri kati ya watumishi wa chini na viongozi.

Michezo iliyofanyika kati ya pande hizo mbili za Muungano kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ni mpira wa Miguu, pete na kuvuta kamba, ambapo mpira wa Miguu Zanzibar iliibuka kidedea kwa goli mbili kwa moja, kuvuta kamba Hazina Sport Club iliibuka mshindi kwa timu ya wanaume na wanawake wakati mpira wa pete Hazina Spot Club ilishinda gori 24 kwa 16 dhidi ya Chuo cha Mipango Dodoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here