Home BUSINESS MHE. KIGAHE AZINDUA JENGO LA UTAWALA LA KIWANDA CHA MATI SUPER BRAND...

MHE. KIGAHE AZINDUA JENGO LA UTAWALA LA KIWANDA CHA MATI SUPER BRAND LTD NA BIDHAA YA TANZANITE PREMIUM VODKA BABATI MKOANI MANYARA

MANYARA.

Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amewahakikishia wawekezaji wote nchini mazingira bora ya uwekezaji ikiwa ni pamoja kutatua changamoto zinazowakabili.

Hayo yamesemwa leo tarehe 30 Aprili, 2022 Babati Mkoani Manyara na Naibu Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Utawala la kiwanda cha Mati Super brand ltd na bidhaa mpya ya Tanzanite premium Vodka.

Mhe. Kigahe amempongeza mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho ambaye ni mwekezaji mzawa Bw. David Mulokozi kwa uamuzi wake wa kujenga kiwanda katika kata ya Bagara ziwani eneo la korongo mbili wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara kwani kimesaidia ajira zaidi kwa wakazi wa Mkoa wa Manyara na kuchangia pato la taifa kwani kiwanda hiki kimeajiri wafanyakazi 216 ambapo ajira za kudumu ni 88 na zisizo za kudumu ni 128 na kinalipa kodi ya serikali kwa maendeleo ya taifa letu.


“Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini ikiwa pamoja na kujenga majengo ya viwanda katika mikoa yote nchini pamoja na kuendeleza maeneo yaliyotengwa ikiwa ni pamoja na kuyawekea miundombinu stahiki kwa ajili ya uwekezaji. Sambamba na juhudi hizo, Serikali kupitia Taasisi ya SIDO, itaendelea kutoa huduma mbalimbali za kuendeleza biashara (BDS) ambazo ni pamoja na huduma za ughani na ushauri, taarifa (kupitia Vituo vya Taarifa vya SIDO na TANTRADE), mafunzo, upatikanaji masoko na teknolojia kupitia viatamizi na karakana za SIDO pamoja na taasisi za TEMDO, CAMARTEC, TIRDO na COSTECH ambazo zinasaidia kusambaza teknolojia rahisi vijijini.” Amesema Mhe. Kigahe.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Mati Super brand ltd Ndugu David Mulokozi Amesema kuwa kiwanda kilisajiliwa Mwezi Oktoba mwaka 2017 na kuanza shughuli za uzalishaji rasmi mwaka 2018 na kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha lita 6,000 hadi 7,200 kwa siku ambazo ni sawa na zaidi 160,000 kwa mwezi au zaidi ya lita 1,900,000.00 kwa mwaka.

Bw. Mulokozi Ameongeza kwa kusema anaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia viongozi wa mkoa wa Manyara na Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa ushirikiano anaopata katika utatuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya barabara ambapo imesababisha kukwama kwa magari ya kiwanda kipindi cha mvua.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Lazaro Twange akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Makongoro Nyerere Amesema kuwa serikali ya Mkoa wa Manyara imetenga maeneo ya kutosha katika Wilaya zote kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa nje hivyo kuwhimiza wawekezaji popote walipo Duniani wafike kuwekeza katika Mkoa wa  Manyara.


Mhe. Twange ameongeza kuwa serikali ya Mkoa wa Manyara imeendelea kuboresha miundombinu ikiwemo ya barabara na sasa barabara, umeme na maji kwa ajili ya kurahisisha uwekezaji Mkoani Manyara.

“Nimshukuru sana rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwani alitupatia fedha ambazo tayari mkandarasi ameanza kazi ya ujenzi wa barabara inayotoka barabara kuu ya Babati kuelekea kiwandani hapa hivyo kero hii ya mwekezaji wa kiwanda hiki cha Mati – Super Brand inaenda kumalizwa na kuwa historia” Amesema Mhe. Twange.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here