Home LOCAL KINANA APITISHWA KWA KURA ZOTE, AWATAKA VIONGOZI KUSIMAMIA HAKI, DEMOKRASIA

KINANA APITISHWA KWA KURA ZOTE, AWATAKA VIONGOZI KUSIMAMIA HAKI, DEMOKRASIA

 Na:Hughes Dugilo.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM wamempitisha kwa kura zote Ndugu Abdullhaman Kinana kuwa Makamo wa Mwenyekiti wa Chama hicho katika Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho uliofanyika leo April 1-2022 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Akitangaza Matokeo ya uchaguzi huo Msimamizi maalum wa kamati ya uchaguzi huo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackoson alitangaza kuwa jumla ya wajumbe wote 1875 waliohudhuria katika mkutano huo wamepiga kura ya ndio na kwamba  hakukuwa na kura  iliyoharibika.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa rasmi kuwa Makamo wa Mwenyekiti wa Chama hicho Ndugu Abdullhaman Kinana amemshukuru Mwenyekiti wa Chama hicho Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzani Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha imani kubwa kwake kwa kupendekeza jina lake kwa Kamati kuu na Halmashauri Kuu ya Chama hicho na hatimaye kupitishwa na kuletwa kwenye Mkutano Mkuu kwaajili ya kupigiwa kura.

Aidha Ndugu Kinana ameeleza mambo matatu ambayo atakwenda kuyafanyia kazi kwa umakini na kujitoa akiamini kuwa chama hicho kinakwenda kufanya kazi zake kwa haki na kwa mujibu wa Katiba, kanuni na taratibu zilizopo.

Ameeleza kuwa katika mambo hayo matatu ni pamoja na kukiimarisha Chama, kiwe imara kinachokubalika kwa wananchi. ” Ndugu Mwenyekiti ili Chama kiwe imara lazima tusimamie Demokrasia ndani ya Chama, kusimamia haki ndani ya Chama, bila mizengwe, bila rushwa na bila kuangalia umaarufu wa mtu”

“Haki ya kutoa mawazo ni jambo muhimu sana ndani ya Chama chetu, lazima kila mwanachama awe huru kutoa mawazo hakuna mwenye haki miliki ya kutoa mawazo, hata uamuzi ukifikiwa na hukuupenda basi kuwe na staha kwa kuheshimu maamuzi yaliyopo”

“CCM sio mali ya Serikali, Serikali hizi zinatokana na CCM, kazi yetu ni kusimamia Serikali kwani kazi ya kusimamia sera, irani na maelekezo, ni kazi ya Chama cha Mapinduzi, pale Serikali inapofanya vizuri kila mwana CCM ana wajibu wa kuisifia na ikitokea tofauti tuna wajibu wa kuikosoa na tusikosoe kwa kufoka, tuziunge mkono Serikali zetu lakini si sawa kuona kila mwana CCM anatoka na kuisema Serikali vibaya” amesema Kinana.

Aidha amesema kuwa CCM ni chama chenye historia kubwa na kwamba kinakubalika, hivyo kuwataka viongozi katika ngazi zote kupenda kuwatembelea wananchi kweye maeneo yao kwa lengo la kujua shida zao kwani kwa kufaya hivyo watazidi kukipenda na kuendelea kukichagua wakitambua kuwa Chama chao kinawajali, kinawapenda na kuwasikiliza.

Awali akizungumza katika hotuba yake ya kuwaaga wanachama wa Chama hicho Makamo Mwenyekiti aliyeng’atuka Mzee Philip Mangula amemshukuru Mwenyekiti wa Chama hicho Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo wameshirikiana na kufanyanae kazi kwa mshikamano mkubwa,

Pia ameishukuru Kamati Kuu ya Chama hicho na Halmashauri kuu kwa ushirikiano wao kwa wakati wote wa kipindi chake cha uongozi  na kwamba kung’atuka kwake haimaanishi kuwa anaondoka kwenye chama bali ataendelea kufanyakazi katika Baraza la ushauri la viongozi wastaafu kama inavyoelezwa katika Ibara ya 22 ya ilani ya CCM.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here